Iraq yadhibiti asilimia 70 ya Tal Afar
26 Agosti 2017Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Iraq imeeleza kuwa majeshi yake yameukomboa mji wa Tal Afar ambao ni muhimu sana kwa sababu uko katika njia inayotumika kusafirisha mahitaji ya IS kati ya Syria na mji wa Mosul ambao ulikuwa ngome muhimu ya IS.
Kamanda wa operesheni za kijeshi, Jenerali Abdulamir Yarallah amesema wanajeshi wa kitengo cha kupambana na ugaidi wameikomboa ngome hiyo na wilaya ya Basatin na wamepandisha bendera ya Irak kwenye maeneo hayo.
Kamanda huyo amesema mashambulizi ya anga na ardhini kwa ajili ya kuukomboa mji wa Tal Afar ulioko kilomita 70 magharibi mwa Mosul, yalianza Agosti 20, 2017.
Hadi wapiganaji 2,000 wanaaminika walikuwa wanapambana kuendelea kuudhibiti mji huo wakati kampeni inayoongozwa na Marekani ya kuikomboa Tal Afar. Kwa mujibu wa duru za jeshi la Marekani na Iraq, inakadiriwa kuwa wanajeshi 50,000 walikuwa wakipambana na IS.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Ibrahim al-Jaafari amesema leo kuwa asilimia 70 ya mji wa Tal Afar umekombolewa kutoka kwa wapiganaji wa IS.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian na Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Paryl, amesema eneo lililobakia litakombolewa hivi karibuni.
Le Drian na Parly ambao wako ziarani kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad, wanatarajia kusisitizia nia ya Ufaransa kuiunga mkono Iraq katika mapambano dhidi ya IS.
Katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, leo mjini Baghdad, Le Drian ametangaza kuwa Ufaransa itaipatia Iraq mkopo wa Euro milioni 420. Amesema uchumi wa Iraq umeshuka kutokana na bei ya mafuta kuwa chini na mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi. Waziri huyo amesema fedha hizo zitatolewa kabla ya mwishoni mwa 2017
Iraq inakabiliwa na changamoto
Akizungumza akiwa njiani kuelekea Iraq, Le Drian amesema Iraq inakabiliwa na changamoto mbili, moja ikiwa ni vita ambavyo vinakaribia kumalizika na kuanza kuijenga tena nchi hiyo na kuhakikisha utulivu wa kudumu unakuwepo.
Mawaziri hao pia watakutana na kiongozi wa Kikurdi wa Iraq, Massud Barzani mjini Arbil, ambako wito umekuwa ukitolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis kwa ajili ya kuahirisha kura ya maoni kuhusu uhuru wake, ambayo imepangwa kufanyika mwezi ujao.
Ufaransa ni mwanachama muhimu katika muungano wa nchi zinazoviunga mkono vikosi vya Iraq katika kampeni ya kuyakomboa maeneo makubwa ya Iraq ambayo yaliangukia kwa wapiganaji wa jihadi wakati wa mashambulizi ya 2014.
Ufaransa imesema raia 700 wa Ufaransa wanapigana katika vita dhidi ya IS nchini Syria na Iraq, ambako kiasi ya wapiganaji wa jihadi 300 wa Ufaransa wameuawa tangu 2014.
Mashirika ya kutoa misaada hayatazamii kuona idadi kubwa ya watu wakiondoka sawa na ile iliyoshuhudiwa wakati wa mashambulizi ya kuukomboa mji wa Mosul. Shirika la kimataifa la Uhamiaji, IOM, limesema kuwa kati ya raia 10,000 na 40,000 wanaaminika kuwepo Tal Afar na maeneo yanayozunguka.
Agosti 22, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR lilisema watu ambao wamekuwa wakikimbia wanakabiliwa na ukosefu wa maji mwilini na uchovu na wamekuwa wakishindia mikate na maji machafu kwa muda wa miezi mitatu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Zainab Aziz