1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yadai kuhusika na shambulizi la bomu Uganda

25 Oktoba 2021

Kundi la Dola la Kiislamu - IS limedai kuhusika na shambulizi la bomu lililomuuwa mtu mmoja katika mji mkuu wa Uganda Kampala Jumamosi usiku.

https://p.dw.com/p/428Q2
Uganda I Explosion in Kampala
Picha: Hajarah Nalwadda/XinHua/picture alliance

Kundi hilo la itikadi kali limesema katika taarifa iliyochapishwa jana usiku kwenye chaneli ya Telegram inayohusishwa nalo.

Kundi hilo lilisema baadhi ya wafuasi wake walifyatua bomu katika baa ambayo wanachama na majasusi wa serikali ya Uganda walikuwa wanakusanyika mjini Kampala.

Polisi ilisema jana bomu hilo, liliulenga mgahawa unaouzwa nyama ya nguruwe viungani vya mji mkuu.

Mlipuko huo ulimuuwa mhudumu wa kike mwenye umri wa miaka 20 na kuwajeruhi watu watatu, wawili wakiwa katika hali mbaya.

Polisi imesema dalili zote zinaashiria kilikuwa ni kitendo cha ugaidi wa ndani.

Uchunguzi uliokusanywa ulionyesha kuwa wanaume watatu, waliojifanya kuwa wateja, waliweka mfuko wa plastiki chini ya meza na kuondoka muda mfupi kabla ya mripuko.