ISLAMABAD: Waliojificha msikitini watoke au watauawa
7 Julai 2007Matangazo
Rais Pervez Musharaff wa Pakistan ameonya kuwa watu waliojificha ndani ya Msikiti Mwekundu mjini Islamabad,watauawa ikiwa hawatotoka nje ya uwanja wa msikiti huo.Kwa upande mwingine,shehe anaesimamia msikiti huo unaofuata itikadi kali za Kiislamu amesema,yeye na wafuasi wake wana silaha na chakula cha kuwatosha mwezi mzima. Akaongezea kuwa wanafunzi 70,ikiwa ni pamoja na wanawake 30 wameuawa,tangu msikiti huo kuzingirwa na polisi kuanzia siku ya Jumanne. Serikali lakini inasema,idadi ya watu waliouawa katika mapambano yaliyozuka ni 19.