1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel haitawaachia huru wafungwa wa kipalestina

4 Aprili 2014

Israel imeufuta mpango wa kuawachia wafungwa wa kipalestina na kudidimiza zaidi matumaini ya kufanikiwa kwa mchakato wa kutafuta amani Mashariki ya kati huku Israel na Palestina zikichukua misimamo mikali

https://p.dw.com/p/1BbmR
Picha: Reuters

Waziri wa sheria wa Israel ambaye pia ndiye mpatanishi mkuu wa nchi yake Tzipi Livni, hapo jana amewaambia wajumbe wa Palestina wa mchakato wa kutafuta amani kuwa Israel haiwezi kuwaachia huru wafungwa 26 kwa sababu Palesetina imeamua kuanza harakati za kutambulika zaidi kimataifa.

Duru zinasema Israel inaichukulia hatua hiyo ya Palestina kama kinyume na makubaliano ya awali ambapo Palestina ilikuwa imeahidi haitaendeleza kampeini zake za kutaka kutambulika kama taifa huru na kujiunga na mashirika na mikataba ya kimataifa inayotambulika na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha pande hizo mbili zinasalia katika meza ya mazungumzo, amewataka wanasiasa wa Israel na Palestina kuonyesha ukomavu na muelekeo wa uongozi katika kushughulikia mchakato huo wa kutafuta amani.

Israel na Palestina zavutana

Mazungumzo hayo yalikwama mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Israel kukataa kuwaachia huru wafungwa wa kipalestina siku ya Jumamosi kama ilivyokuwa imetarajiwa na kuighadhabisha Palestina ambayo Rais wake Mahmoud Abbas aliwasilisha maombi ya kutaka nchi hiyo kujiunga na mashirika ya kimataifa takriban 15 yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: Reuters/Mohamad Torokman

Livni ameitaka Palestina kufutilia mbali uwasilishwaji huo wa kutambulika kimataifa na kurejea mara moja katika meza ya mazungumzo lakini Palestina imesisitiza kuwa haitafanya hivyo hadi kuwe na marekebisho katika makubaliano yaliyofikiwa awali na Israel ambayo inaishutumu kwa kugeuka na kutoheshimu mikataba.

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Marekani Jay Carney amesema uamuzi wa Israel wa kutowaachia huru wafungwa wa kipalestina unaibua changamoto na kuzorotesha juhudi za kupatikana ufumbuzi katika mzozo huo wa muda mrefu wa mashariki ya kati:

Hata hivyo Carney amesema Kerry na kundi la wajumbe wa Marekani wanaoshiriki katika mchakato huo hawatakatishwa tamaa na changamoto hizo na watajaribu kuhakikisha pande zote mbili zinaendelea kushiriki katika mazungumzo.

Marekani yasikitishwa na hatua za pande zote mbili

Kerry ambaye amekua katika pilika pilika za juu chini kwa takriban mwaka mzima kushughulikia mchakato huo wa kupatikana amani amewapigia simu waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Abbas lakini yaliyojadiliwa hayajawekwa wazi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Huku hayo yakijiri,wapalestina katika ukanda wa Gaza wamefyatua makombora manne kusini mwa Israel na kujibiwa mara moja kwa mashambulizi ya angani kutoka Israel.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema hakuna aliyejeruhiwa katika majibizano hayo ya leo.Maafisa wa usalama wa Palestina wamethibitisha kuwa Israel imelishambulia eneo la Gaza leo ikilenga vituo sita vya kundi la Hamas tawi la kijeshi katika mji wa Gaza.

Mwandishi:Caro Robi/AFP

Mhariri: Gakuba Daniel