1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Tumemuua kamanda mwingine wa Hezbollah, Kaouk

Hawa Bihoga
29 Septemba 2024

Jeshi la Israel pia limetangaza kumuua kamanda mwingine mwandamizi wa Hezbollah, Nabil Kaouk. Hezbollah haijazungumzia hatma ya Kaouk, lakini salamu za maombolezo zimekuwa zikichapishwa mitandaoni na wafuasi wake.

https://p.dw.com/p/4lCgx
Lebanon | Israel | Makaazi ya raia yakiwa yameharibiwa kwa mashambulizi Beirut
Majengo ya makaazi ya raia Lebanon yakiwa yameharibiwa kwa mashambulizi ya IsraelPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Katika hatua nyingine shambulio la anga la Israel Kaskazini mashariki mwa Lebanon limeuwa watu 11 leo Jumapili, ikiwa ni siku moja baada ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah kuthibitisha kifo cha makamanda wake kadhaa akiwemo kiongozi wake wa muda mrefu Hassan Nasrallah.

Soma pia:Hezbollah yaahidi kulipiza kisasi baada ya kuuliwa kiongozi wake

Hezbollah na Israel zimekuwa zikishambuliana karibu kila siku tangu kuzuka kwa vita vya Israel na Hamas mnamo Oktoba 7, kwa kile Hezbollah inasema kuonesha mshikamano kwa Gaza.

Nchini Iran ambayo ni mshirika mkuu wa kundi la Hezbollah kumeshuhudia maandamano makubwa yakilaani na kupinga mauaji ya kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah kwenye shambulio la Israel. Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu waliokimbia mzozo kusini mwa Lebanon imeongezeka zaidi ya maradufu.

Mapema leo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema limeanzisha operesheni ya dharura ya kutoa chakula kwa watu milioni moja walioathiriwa na mzozo huo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.