UNICEF "Gaza eneo hatari zaidi kwa watoto"
19 Desemba 2023UNICEF linasema haya wakati Shirika la Afya, WHO likisema hali mbaya kabisa kwenye eneo hilo haijashuhudiwa bado mahala popote ulimwenguni.
Wakiwa mjini Geneva, wasemaji kutoka UNICEF, James Elder na Margareth Harrison, wamezungumzia hali mbaya katika Ukanda wa Gaza tangu israel ilipoanzisha mashambulizi ya kisasi dhidi ya kundi la Hamas lililoishambulia kwanza mnamo Oktoba 7.
Elder amesema Gaza ni mahala pa hatari zaidi ulimwenguni kwa sasa na hapafai kwa watoto kuishi. Elder aliyerejea Geneva akitokea Gaza, amesema hayo huku akieleza kuchukizwa na viongozi ambao amesema hawajali namna ambavyo watoto wanaathirika kutokana na mashambulizi hayo.
Elder alisema "Nina hasira. Nina hasira kwamba wale walio na mamlaka wanapuuzia wakati jinamizi la kibinadamu linalowatafuna watoto milioni moja. Nina hasira kwamba watoto wanaopona majeraha baada ya kukatwa viungo wanauawa wakiwa hospitalini."
Soma pia: Papa Francis aomboleza kifo cha "raia wasio na ulinzi" ukanda wa Gaza
Alikuwa akiwazungumzia watoto waliokatwa viungo na baadae kuuawa wakiwa kwenye hospitali ambazo pia zilishambuliwa. Amesema hospitali ya Nasser ambayo pekee ndio iliyokuwa ikiendelea kutoa huduma, katika mji mkuu wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis imeshambuliwa mara mbili katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita. Alisema "Nina hasira kwamba kuna watoto zaidi ambao sasa wamejificha mahali fulani ambao bila shaka watapigwa na kukatwa viungo siku zijazo."
Hospitali ya Nasser ilikuwa ikihifadhi watoto na wanawake
Hospitali hiyo kulingana naye, sio tu ilikuwa inahifadhi idadi kubwa ya watoto ambao tayari walikuwa wamejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa majumbani kwao, bali pia mamia ya wanawake na watoto waliokuwa wakitafuta mahala salama pa kujihifadhi.
Lakini si yeye tu aliyezungumzia madhila yanayowakumba watu wa Gaza, bali pia msemaji wa shirika la Afya ulimwenguni, Margareth Harrison alisema hata wafanyakazi wenzake wanakiri kwamba hawajawahi kushuhudia kile kinachoendelea sasa kwenye eneo hilo la Palestina.WHO
Harrison alisema "Mfanyakazi mwenzangu alituambia watu walikuwa wamelala sakafuni wakiwa na maumivu makali, wakiwa na uchungu...lakini hawakuomba dawa ya kutuliza maumivu. Walikuwa wakiomba maji."
Wizara ya afya ya Gaza yasema shambulizi la Israel liliwaua watu 20
Wizara ya Afya ya Gaza imesema kwamba shambulizi la Israel liliwaua watu 20 huko Rafah. Na Shirika la habari la AP liliripoti likiwanukuu waandishi walioko huko kwamba shambulizi katika makazi yaliyowahifadhi raia lilisababisha vifo vya karibu watu 25.
Na taarifa kutoka huko Israel zimesema mapema leo kwamba kulisikika ving'ora vya tahadhari katika mji wa Tel Aviv baada ya wanamgambo wa Hamas kusema walirusha mkururo wa maroketi kuelekea kwenye mji huo wa pwani.
Ving'ora pia vililia katika miji ya Jaffa, Bat Yam, Rishon Lezion, Kfar Chabad na Beit Dagan. Jeshi la Israel, IDF, liliandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba hata baada ya siku 74 za vita dhidi ya Hamas, ving'ora vimesikika katikati mwa Israel na mamilioni ya Waisrael walikimbilia mafichoni.
Hata hivyo hakukua na ripoti za uharibifu yoyote.
Kundi la Hamas, limeorodheshwa na Israel, Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kuwa ni la kigaidi.