Israel itaondoa maelfu ya askari katika ukanda wa Gaza
2 Januari 2024Hata hivyo, licha ya mashambulizi hayo, jeshi la Israel limethibitisha jana kuwa litawaondoa maelfu ya askari wake kutoka ukanda wa Gaza katika wiki zijazo.
Licha ya shinikizo la kimataifa la kutaka vita hivyo kusitishwa, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari ameeleza kuwa jeshi la nchi hiyo linajiandaa kwa "mapigano ya muda mrefu" yanayotarajiwa kudumu mwaka huu wote 2024.
Usiku wa kuamkia leo, mashuhuda wamesema makombora yalirushwa kuelekea mji wa Rafah upande wa kusini na karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabalia upande wa kaskazini. Mapigano pia yameripotiwa karibu na maeneo ya kati ya Maghazi na Bureji pamoja na mji wa Khan Yunis, ulioko upande wa kusini mwa Gaza.
Soma pia: Mashambulizi ya Israel yauwa 35 Gaza
Kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miezi mitatu vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 22,000 na kuharibu sehemu kubwa ya eneo lililozingirwa.
IDF: Jeshi la Israel limewaua wanamgambo watano wa Kipalestina
Wakati hayo yanaarifiwa, jeshi la Israel limesema wanamgambo watano wa Kipalestina wameuawa katika tukio la ufyatulianaji risasi katika eneo linalokaliwa kimabavu la ukingo wa magharibi.
Hata hivyo, hakujatolewa kauli yoyote kutoka kwa maafisa wa Palestina juu ya vifo hivyo.
Soma pia: UN: Hatari ya uhalifu wa kivita ni kubwa Gaza
Taarifa kutoka jeshi la IDF imeeleza kuwa, wanajeshi wake wamewaua kwa kuwapiga risasi wanamgambo wanne waliowafyatulia risasi kutoka ndani ya nyumba moja ilioko kijiji cha Azzun, na kwamba mwanajeshi mmoja wa Israel amejeruhiwa katika tukio hilo.
Na katika tukio lengine huko Qalqiya, wanajeshi wa Israel walimpiga risasi na kumuua mwanamume mmoja aliyekuwa amejihami kwa silaha wakati jeshi hilo lilipokuwa kwenye msako wa kukamata silaha.
Brigedi tano za kijeshi zitaondolewa kutoka Gaza
Ama kwa upande mwengine, taarifa ya kupunguzwa kwa idadi ya wanajeshi wa Israel katika ukanda wa Gaza imetolewa siku moja sambamba na uamuzi wa mahakama ya juu ya nchi hiyo kutupilia mbali kipengele muhimu cha mpango wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, mpango wenye utata kuhusu mageuzi katika idara ya mahakama.
Licha ya mpango huo wa Netanyahu kutokuwa na mafungamano ya moja kwa moja na vita vinavyoendelea huko Gaza, unatajwa kuwa ndio chanzo cha mgawanyiko ndani ya Israel.
Wanasiasa nchini humo wametahadharisha juu ya kuchochea migawanyiko zaidi na kuathiri mshikamano wa kitaifa ambao unaonekana imara katika kipindi chote cha vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas.
Soma pia: WHO yatoa wito wa kupunguza mateso ya watu wa Gaza
Katika tangazo lake, Israel imesema itaondoa brigedi tano za kijeshi kutoka ukanda wa Gaza katika wiki zijazo.
Daniel Hagari amesema, "Siku hizi, tunaufanyia mabadiliko mpango wa kupeleka vikosi katika ukanda wa Gaza hasa askari wetu wa akiba. Baadhi yao watarejea kwa familia zao na kuendelea na kazi zao za kawaida wiki hii."
Inaarifiwa kuwa baadhi ya askari watarudi kwenye kambi ili kupokea mafunzo zaidi au kupumzika huku wengine, hasa askari wa akiba wenye umri mkubwa watarudi majumbani mwao.
Msemaji wa jeshi Daniel Hagari hata hivyo hakuweza wazi iwapo hatua ya kuondolewa kwa baadhi ya wanajeshi huko Gaza ni ishara ya awamu mpya ya vita.