Israel kupokonya ekari 370 za ardhi Palestina
21 Januari 2016Ardhi hiyo ya mashamba ipo katika Bonde la Jordan kusini mwa mji wa Jericho, na kwa mujibu wa shirika la kutetea makaazi la Peace Now, huu ni ukamataji wa ardhi mkubwa kutokea tangu ule wa hekta 400 mwaka 2014. Shirika hilo limeongeza kuwa uamuzi huu wa serikali ya Israel utarejesha nyuma uwezekano wa pande hizo mbili kupata suluhisho la tofauti zao.
Mkuu wa ujumbe wa mazungumzo wa Palestina, Saed Erekat, amelitembelea aneo hilo jana, na kusema wanachokifanya Waisrael ni kuiba ardhi ya Wapalestina.
"Tunawasiliana na jumuiya ya kimataifa, Wamarekani, Wazungu, na wengineo. Tunataka ushauri wao kwa sababu nadhani tunapaswa kwenda Baraza la Usalama na azimio la kupinga makaazi ya kikoloni. Na kwa wale ambao wanaotuzuia tusiende Baraza la Usalama, basi kwanza waambieni Waisrael waachane na makazi yetu, lakini hawatokusikilizeni. Wahamsikilizi Rais wa Marekani Barack Obama, hawamsikilizi waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, hawamsikilizi Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, hawamsikilizi mtu yeyote. Hivyo tafadhalini, tunaomba tuachiwe tuende Baraza la Usalama na azimio linalohusu shughuli za makazi, msituzuie, sisi ndio waathirika hapa," amesema Saed Erekat.
Eneo lenye utata
Israel iliteka eneo la Ukingo wa magharibi kutoka Jordan wakati wa vita vya mwaka 1967. Wapalestina wanadai kwamba eneo hilo ni lao. Na jumuiya nzima ya kimataifa inakubaliana na Wapalestina kwamba makaazi ya Israel kwenye eneo hilo ni kinyume na sheria.
Israel nayo inadai kwamba hatima ya makaazi hayo lazima ijadiliwe katika mazungumzo ya amani, pamoja na masuala mengine muhimu kama vile usalama na mipaka.
Kwa upande wa Marekani, msemaji mkuu wa wizara ya mamabo ya nje ,Mark Toner, ameilaani hatua hiyo. Mark alisema Marekani inapinga hatua yoyote itakayoongeza kasi, upanuzi wa makaazi ya Waisrael katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi, na kwamba haiendani na suluhisho la kuundwa kwa nchi mbili, na wanaitilia shaka dhamira ya Israel ya kulikubali suluhisho la kuundwa kwa nchi mbili.
Baraza la ulinzi la Israel la COGAT limesema kwamba uamuzi huwo wa kuchukua ardhi ulifanywa na viongozi waandamizi wa Israel na kwamba upo katika hatu za mwisho za utekelezaji.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef