1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Palestina zaanza mazungumzo

9 Machi 2010

Waisrael na Wapalestina wameanza mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliyopita

https://p.dw.com/p/MNgJ
Makamau wa Rais wa Marekani JoePicha: Fena

Kufanyika kwa mazungumzo hayo kulitangazwa na Marekani, kunakuja mnamo wakati ambapo Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden leo akiwa katika siku yake ya pili ya kuzuru Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Philip Crowley amethibitisha kuanza kwa mazungumzo hayo chini ya upatanishi wa mjumbe maalum wa nchi hiyo huko Mashariki ya Kati George Mitchell.

Msemaji huyo amesema, George Mitchell ameondoka Mashariki ya Kati kwenda Washington kumuarifu Waziri wa Nje Hillary Clinton juu ya maendeleo ya hatua hiyo.Mitchell alikutana kwanza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kabla ya kuelekea Ramallah ambako alikuwa na mazungumzo Rais wa mamlaka ya wapalestina Mahamoud Abbas.

Hii ni mara ya kwanza kwa pande hizo mbili kuingia katika mazungumzo ya amani kwenye eneo hilo, tokea Israel ilipoanzisha mashambulizi ya siku 22 dhidi ya Ukanda Gaza mwaka jana, katika kile ilichosema, kukomesha mashambulio ya maroketi kutokea Gaza.

Lakini wakati hayo yakiendelea Wapalestina wameelezea kukasirishwa kwao na hatua ya Israel kuidhinisha ujenzi wa nyumba mpya 112 katika makaazi ya walowezi wa kiyahudi kwenye maeneo inayoyakalia ya Ukingo wa Magharibi.

Mpatanishi mkuu wa mamlaka ya Palestina Saeb Erekat amesema kuwa mazungumzo hayo ni jaribio la mwisho katika kufufuliwa kwa mazungumzo ya amani , na kuonya juu ya hatua hiyo ya Israel kujenga nyumba zaidi.

Palästinensischer Präsident Abbas mit Saeb Erekat in Kairo
Seb Erekat kushoto na Rais wa Ppalestina Mahmoud Abbas kulia.Picha: picture alliance/dpa

´´Kutakuwa na madhara makubwa, iwapo Mitchell atakubali, kwani kutakuwa na makaazi zaidi ya walowezi,kutakuwa na masharti zaidi, na hivyo kuwepo na swali kubwa la jinsi ya kuendelea na mazungumzo.Tunalaani hatua hii ya Israel na tunaitaka Marekani kuzuia kabisa hatua hii, ili kutoa nafasi kwa amani kuchukua nafasi yake´´

Hata hivyo Marekani imeunga mkono ujenzi huo, ambapo msemaji wa wizara ya nje ya nchi hiyo Philip Crowley amesema hatua hiyo haivunji makubaliano ya kuchelewesha ujenzi zaidi wa makaazi ya walowezi, lakini akaonya kuwa ni suala ambalo pande zote mbili zinatakiwa kuliangalia kwa umakini mnamo kipindi hiki cha kuelekea katika kufufuliwa kwa mazungumzo.

Naye Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amewasili huko Mashariki ya Kati, ambapo leo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na viongozi wa Israel, kabla ya kwenda Ramallah kukutana Rais wa Mamlaka yaPalestina Mahamoud Abbas.

Anategemewa kuongeza uzito katika hatua ya kufufuliwa kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Palestina.Pia suala la mpango wenye utata wa nyuklia wa Iran litakuwa katika ajenda yake kwenye mazungumzo hayo.

Ban Ki-moon auf Kopenhagener Klimagipfel
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mkuu wa Israel Silvan Shalom amemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kusaidia juhudi za kufufuliwa kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Palestina.

Amemuomba kushawashi washirika wa umoja huo katika kundi la pande nne la kutafuta amani ya Mashariki ya Kati, katika mkutano wao wa wiki ijayo mjini Moscow.Mbali ya Umoja wa Mataifa nyingine zilizoko katika kundi hilo ni pamoja na Umoja wa Ulaya, Urusi na Marekani.

Israel pia imetangaza kuwa imewaruhusu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pamoja na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton kuingia Ukanda wa Gaza.Eneo hilo limezungukwa na Iisrael ambayo imeweka vizuizi vya kuingia.Bibi Ashton anatarajiwa kwenda Ukanda wa Gaza Jumapili ijayo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/DPA/Reuters

Mhariri:Othman Miradji