Watu saba wauliwa katika shambulio Jerusalem Mashariki.
28 Januari 2023Mshambukliaji huyo wa kipalestina alifyatua risasi na kuwaua watu hao saba. Watu wengine watatu walijeruhiwa katika shambulio hilo miongoni mwao ni mwanamke mwenye umri wa miaka 70. Polisi walimpiga risasi na kumwuua mpalestina huyo. Kamishna wa polisi, Kob Shabtai amesema mshambuliaji huyo alitambuliwa kuwa mkaazi wa Jerusalem mashariki aliyekuwa na umri wa miaka 21 na kwamba mtu huyo alifanya kitendo hicho peke yake.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema baraza lake la usalama litatangaza hatua za haraka za kujibu shambulio hilo. Mkasa huo umetokea katika muktadha wa mvutano unaozidi kupamba moto baina ya Israel na wapalestina.
Siku moja kabla ya hapo wapalestina 9, wakiwemo wapiganaji na mama mmoja mzee waliuliwa katika shambulio lililofanywa na wanajeshi wa Israel kwenye mji wa Jenin wa sehemu ya Ukingo wa Magharibi inayokaliwa na Israel.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karine Jean-Pierre amesema Marekani imelaani vikali shambulio hilo na imeshtushwa na kuhuzunishwa na tukio la watu kupoteza maisha, ikibainisha kuwa limetokea wakati wa Kumbukumbu ya Kimataifa ya wayahudi na watu wengine wote waliongamizwa na utawala wa manazi wakati wa vita vikuu vya pili.
Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutoa pole za watu wa Marekani kwa serikali na watu wa Israel. Biden ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni mashambulizi dhidi ya ustaarabu wa dunia na wakati huo huo amesema Marekani itatoa kila aina ya msaada utakaohitajika kwa serikali na watu wa Israel katika siku zijazo.
Balozi wa Ujerumani nchini Israel, Steffen Seibert amelaani shambulizi hilo na ametoa rambirambi zake kwa familia za wahanga. Seibert ameandika kwenyee ukurasa wake wa Twitter kama ifuatavyo:
"Nimehuzunishwa sana na ripoti kuhusu mshambuliaji wa Kipalestina aliyewaua waumini karibu na Sinagogi usiku wa Ijumaa katika eneo la Neve Yaakov - kitendo kiovu cha kigaidi dhidi ya Wayahudi katika Siku ya Kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi. Moyo wangu unawakumbuka familia za watu waliouawa na ninawaombea afya wale waliojeruhiwa. "
Vyanzo:AFP/AP/DW