Israel yaanza mwaka mpya chini ya misururu ya makombora Gaza
1 Januari 2024Vita katika Ukanda wa Gaza vimeendelea mwaka huu mpya leo Jumatatu wakati kundi la wanamgambo wa Hamas liliporusha makombora kueleka Israel muda mfupi baada ya saa sita za usiku na takriban watu 22 kuuawa kutokana na mashambulizi ya usiku kucha ya Israel katika eneo hilo.
Ving'ora vya tahadhari vilisikika kote Israel huku waandishi wa shirika la habari la AFP mjini Tel Aviv wakielezea kushuhudia mifumo ya ulinzi ikitenguwa makombora angani, na watu waliokuwa wakisherehekea kuingia kwa mwaka mpya wakikimbilia usalama wao.
Soma pia: Afrika Kusini yaishtaki Israel ICJ kwa 'mauaji ya kimbari' Gaza
Ezzedine al-Qassam, kikosi chenye silaha cha Hamas, kimedai kuhusika na shambulio hilo katika video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kikosi hicho kimeongeza kuwa kimerusha makombora aina ya M90 "kujibu mauaji ya raia" yaliyofanywa na Israel.
Jeshi la Israel limethibitisha kutokea kwa shambulio hilo bila ya kuripoti kuhusu majeruhi au uharibifu wowote.