1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yadai kuyashambulia maeneo zaidi ya 100 ya Hizbullah

30 Oktoba 2024

Jeshi la Israel linadai kuyashambulia zaidi ya maeneo 100 ya kundi la Hizbullah na kuwauwa wapiganaji wengi wa kundi hilo, huku Hizbullah na jeshi la Ansarullah la Yemen wakirusha makombora na droni kuelekea Israel.

https://p.dw.com/p/4mOOV
Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.Picha: KAWNAT HAJU/AFP

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Israel siku ya Jumatano (Oktoba 30) ilisema kwamba lilikuwa limeyalenga yale iliyoyaita "maeneo ya kigaidi" na kuwaangamiza iliowaita makumi ya "magaidi wa Hizbullah" kwenye maeneo mbalimbali ya Lebanon. 

Vile vile, taarifa hiyo kupitia mtandao wa Telegram ilisema kuwa wanajeshi wa ardhini wa Israel waliendelea na msako wa nyumba kwa nyumba kwenye maeneo ya Hizbullah yaliyo kusini mwa Lebanon.

Soma zaidi: Hezbollah yamtangaza Naim Qassem kuwa kiongozi mpya

Kupitia taarifa hiyo iliyonukuliwa na shirika la habari la Ujerumani, dpa, Israel ilidai kuwa jeshi lake lilikuwa limepata idadi kubwa ya silaha pamoja na kuyaharibu mahandaki yanayotumiwa na Hizbullah kurusha makombora yake kuelekea miji mbalimbali ya Israel. 

Ingawa shirika hilo la habari halikuweza kuthibitisha taarifa hiyo kupitia vyanzo huru kwa haraka, lakini kwa mujibu wa ripoti kutoka Lebanon, raia kadhaa waliuawa kutokana na mashambulizi ya Israel. 

Hizbullah yarusha makombora Israel

Kwa upande wao, wapiganaji wa kundi la Hizbullah walidai kurusha makombora kadhaa kuelekea kaskazini mwa Israel ndani ya masaa 24 yaliyopita. 

Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.Picha: AFP

Mamlaka nchini Israel zilikiri kutokea mashambulizi hayo, ambapo zilisema mtu mmoja aliuawa na baadhi ya majengo kuharibiwa baada ya makombora yapatayo 50 kuvurumishwa kutokea Lebanon, ingawa baadhi yake yalidunguliwa na mfumo wa ulinzi. 

Soma zaidi: Malalamiko makubwa juu ya Israel kulipiga marufuku shirika la misaada la Umoja wa Mataifa

Polisi ya Israel ilisema kuwa ilipokea ripoti kadhaa za makombora yaliyoangukia kwenye mji Maalot-Tarshiha bila kusababisha madhara makubwa. 

Ansarullah washambulia

Kwa upande mwengine, kundi la Ansarullah, maarufu kama Wahouthi nchini Yemen, lilirusha droni kuelekea mji wa viwanda wa Ashkelon nchini Israel siku ya Jumanne (Oktoba 29). 

Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.Picha: MAHMOUD ZAYYAT/AFP

Hayo yalithibitishwa na jeshi la Israel ambalo lilisema ving'ora vililia asubuhi ya Jumanne kwenye mji huo baada ya droni kuingia kwenye anga ya Israel, lakini iliangukia kwenye eneo tupu.

Soma zaidi: Israel yakosolewa kwa kutaka kulipiga marufuku UNRWA

Siku ya Ijumaa, wapiganaji hao wa Yemen walidai kuzishambulia meli tatu kwenye Bahari ya Sham, ambazo walisema zilikuwa na mafungamano na Israel. 

Kampeni ya Ansarullah kuzishambulia meli kwenye eneo hilo ilianza tangu mwezi Novemba 2023, wakidai kuwa wanatekeleza sheria ya kimataifa ya kuwasaidia Wapalestina kuzuwia mauaji ya maangamizi kwenye Ukanda wa Gaza.

Mauaji yaendelea Gaza

Kwenyewe Gaza, jeshi la Israel liliendelea na mashambulizi yake kaskazini mwa Ukanda huo, ambapo zaidi ya watu 100 waliripotiwa kuuawa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Matokeo ya mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Matokeo ya mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: AFP

Mashambulizi ya asubuhi ya Jumatano (Oktoba 30) yaliuwa watu 20, nane kati yao wakiuawa kwenye kitongoji cha Salateen huko Beil Lahiya, karibu sana na eneo ambalo watu 93 waliripotiwa kuuawa au kutojulikana walipo kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya jengo la ghorofa siku ya Jumanne.

Soma zaidi: Shambulio la Israel lauwa Wapalestina kiasi 34 Kaskazini mwa Gaza

Marekani, mshirika na mfadhili mkubwa wa Israel, iliyaita mashambulizi hayo kuwa "ya kuogofya."

Hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa jeshi la Israel, ambalo lilishatangaza kulishinda kundi la Hamas kwenye eneo hilo, lakini baadaye likasema limelazimika "kurejea baada ya wapiganaji hao kujikusanya upya."

Umoja wa Mataifa umeielezea hali kaskazini mwa Gaza kuwa ni kiza kizito.