1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yadaiwa kuwatenga na kuwabagua Wapalestina

27 Aprili 2021

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limedai Israel inatenda uhalifu wa ubaguzi wa rangi na utengano kwa kutaka kuendeleza utawala wa kiyahudi juu ya Wapalestina na raia wake wenye asili ya Kiarabu

https://p.dw.com/p/3sdMW
Human Rights Watch Logo Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Israel ambayo kwa sasa inachunguzwa na Mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC kwa madai ya uhalifu wa kivita imeyakosoa madai ya shirika hilo la Human Rights Watch, na kuyaelezea kama ya kipuuzi na ya uwongo.

Shirika hilo limesema madai yake kwamba Israel inatekeleza uhalifu wa ubaguzi wa rangi na mauaji dhidi ya wapalestina, yametokana na mipango ya serikali ya nchi hiyo na matamshi kutoka kwa maafisa wake.

soma zaidi: ICC yaanza kuchunguza uhalifu katika maeneo ya Wapalestina

Ripoti ya HRW yenye kurasa 213 imeendelea kusema kuwa madai yake yanajikita katika namna Isarel inavyowatendea wapalestina katika eneo linalokaliwa kimabavu la ukingo wa Magharibi, eneo lililozingirwa la Ukanda wa Gaza, eneo lililotwaliwa la Jerusalem Mashariki pamoja na Waarabu wa Isareli, neno linalotumiwa kuwaelezea wapalestina waliobakia katika ardhi ya Israel baada ya dola hilo kuundwa mwaka 1948.

Omar Shakir Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch kwa upande wa Israel na Palestina amesema kumekuwepo na onyo kwa miaka mingi kwamba uhalifu wa ubaguzi wa rangi na utengano - Apartheid, unaonekana katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.

Shirika hilo limetaja kuwawekea wapalestina vizuizi, kuwapokonya ardhi, kuwahamisha kwa nguvu, kunyimwa haki ya kuwa wakaazi wa eneo wanalokalia na kunyimwa haki zao za msingi kama mifano ya uhalifu Israel inaowatendea wapalestina.

Israel yakanusha madai ya shirika la HRW

USA Mittlerer Osten Friedensgespräche Benjamin Netanyahu und Mahmoud Abbas
Kiongozi wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmood Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: CHRIS KLEPONIS/AFP/Getty Images

Hata hivyo wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imesema ripoti ya HRW ni ya propaganda na kulitaja shirika hilo kuwa na mipango ya muda mrefu ya kuisusia Israel.

Taifa hilo kwa muda mrefu limelikalia kimabavu eneo la ukingo wa Magharibi kuanzia mwaka wa 1967 mwaka ambao lilinyakuwa pia eneo la Jerusalem Mashariki. Tangu wakati huo wakaazi wa kiyahudi katika maeneo yote mawili wameendelea kumiliki sehemu kubwa za ardhi. Wapalestina wa maeneo hayo wamekuwa wakinyimwa vibali vya ujenzi huku ujenzi upande wa wakaazi wa kiyahudi ukiendelea.

soma zaidi: Pande pinzani nchini Palestina zaandaa mkutano wa pamoja kuhusu Israeli na UAE

Human Rights Watch imetaka maafisa wote watakaopatikana na hatia ya kufanya uhalifu huo wa kigaguzi dhidi ya watu wa palestina wawekewe vikwazo na mali zao kuzuiliwa.

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa Misri wamesema mamlaka ya wapalestina imepanga kufutilia mbali uchaguzi wake wa kwanza ndani ya miaka 15 kufuatia Israel kukataa uchaguzi kufanyika Jerusalem Mashariki. Misri inasemekana kuwa katika mazungumzo na Israel kukubali uchaguzi ufanyike katika eneo hilo jambo ambalo halina matumaini ya kufanikiwa.

afp/reuters/ap