Israel yaendelea kuihujumu Gaza
22 Julai 2014Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amewasili jana usiku mjini Cairo alikokutana na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo huo unaozidi kuangamiza maisha.
Hata hivyo leo asubuhi jeshi la Israel limesema litaendelea na hujuma zake.
Vyombo vya habari vya Palastina vilizungumzia kwa upande wao uwezekano wa kuwekwa chini silaha kwa muda ili kuwaruhusu wakaazi wa eneo hilo linalozingirwa kujipatia mahitaji yao muhimu. Lakini ripoti hizo hazikuthibitishwa mpaka sasa.
Mjini Doha rais wa mamlaka ya Palastina Mahmoud Abbas alikutana na kiongozi wa Hamas Khaled Mechaal na kudai "yakome mashambulio ya Israel huko Gaza pamoja na kuondolewa vizuwizi vilivyowekwa na Israel tangu mwaka 2006.
"Hamas na Abbas wamekubaliana makundi yote ya wapalastina yanabidi yashirikiane kuunga mkono silaha ziwekwe chini" ameema Azzam al Ahmad wa chama cha Fatah.
"Kwanza silaha lazma ziwekwe chini,baadae tutaendelea kuzungumza na Misri na pande zote zinazohusika kimkoa na kimataifa hadi makubaliano ya amani yanafikiwa.." amesisitiza bwana al Ahmad.
Ban Ki Moon ataka silaha ziwekwe chini haraka
Mjini Cairo,mpatanishi wa jadi wa mizozo kati ya dola hilo la kiyahudi na Hamas,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ametetea "juhudi za haki na zinazofaa" za Israel "kujihami dhidi ya makombora ya wapalasina.Hata hivyo amesema ameingiwa na wasi wasi kutokana na hatima ya raia wa kawaida katika Gaza.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito silaha ziwekwe chini haraka ili kupata njia ya kuwahudumia wahanga,majeruhi na kuwapatia misaada raia.
Leo hii mnamo siku ya 15 ya hujuma za Israel ,wapalastina 7 wameuliwa Gaza kufuatia mashambulio mengine ya madege ya kivita ya Israel.Watao kati yao ni watu wa familia moja. "Wote ni wa familia moja. Baba ni daktari aliyesomea na kupata shahada zakwe nchini Ujerumani na alikuwa na uraia wa Ujerumani." Amesema daktari mmoja wa Gaza.
Tangu hujuma za Israel zilipoanza wapalastina wasiopungua 583 wameuwawa na 3640 kujeruhiwa-wengi kati yao ni raia wa kawaida.
Jeshi la Israel limewapoteza wanajeshi 27- idadi kubwa ya wanajeshi ikilinganishwa na vita vya mwaka 2006 dhidi ya Hisbollah.Wakati huo huo maiti ya mwanajeshi wake mmoja haijulikani iliko huku Hamas wakidai kumteka nyara mwanajeshi mmoja wa Israel.
Amnesty International inadai uchunguzi ufanywe
Jeshi la Israel linaendelea na opereshini zake katika mtaa wa Chajaya ambako wapalastina 70 wengi wakiwa raia wa kawaida waliuliwa hapo awali.
Shirika la Amnesty International linataka uchunguzi wa kimataifa ufanywe kutokana na kuendelezwa hujuma za Israel dhidi ya maeneo wanaoishi raia na hospitali-,hujuma wanazozitaja kuwa ni "uhalifu wa vita.".
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman