1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaendelea kuulenga mji wa Rafah, Ukanda wa Gaza

21 Aprili 2024

Mashambulizi ya usiku kucha ya Israel kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah yamewauwa watu 18, wakiwemo watoto 14.

https://p.dw.com/p/4f1Gl
Mzozo wa Gaza | Rafah
Uharibifu uliotokana na shambulizi la Israel kwenye mji wa Rafah. Picha: Khaled Omar/Xinhua/IMAGO

Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa afya, wakati Marekani ikiidhinisha mabilioni ya dola ya msaada wa ziada wa kijeshi kwa mshirika wake huyo wa karibu. Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani ya karibu kila siku mjini Rafah, ambako zaidi ya nusu ya wakaazi milioni 2.3 wa Gaza wamekimbilia kutokana na mashambulizi kwingineko katika Ukanda huo uliozingirwa.

Shambulizi la kwanza lilimuuwa mwanaume, mkewe na mtoto wao mwenye umri wa miaka mitatu, kulingana na hospitali iliyo karibu ya Kuwait ambayo iliipokea miili hiyo.

Mwanamke huyo alikuwa mjamzito, na madaktari walifanikiwa kumuokoa mtoto. Shambulizi la pili liliwauwa watoto 13 na wanawake wawili, wote wa familia moja kwa mujibu wa rekodi za hospitali. Shambulizi la Rafah usiku uliotangulia, liliwauwa watu tisa, wakiwemo watoto sita.

Wakati hayo yakiendelea Baraza la Wawakilishi la Marekani limeidhinisha msaada wa dola bilioni 26, ambao unajumuisha karibu dola bilioni 9 kwa msaada wa kiutu huko Gaza.