1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya shambulio katika bandari ya Syria

7 Desemba 2021

Israel imefanya shambulio la anga lililolenga shehena ya silaha za Iran katika bandari ya Latakia nchini Syria usiku wa kuamkia leo, shambulio hilo likiwa la kwanza kwenye bandari hiyo.

https://p.dw.com/p/43vb8
Syrien Hafen Latakia
Picha: Mikhail Voskresenskiy/Sputnik/dpa/picture alliance

Shirika la haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema shambulio hilo lililenga shehena ya silaha za Iran. Shirika la habari la serikali ya Syria SANA limeripoti kutokea kwa shambulio hilo katika yadi ya kuhifadhi makontena katika bandari ya Latakia bila ya kutoa maelezo zaidi ya ni nini hasa kilicholengwa.

Shirika hilo la haki za binadamu la Syria, lenye mtandao mpana wa vyanzo vya habari kote nchini Syria, limeongeza kuwa shambulio hilo lilisababisha kutokea kwa milipuko kadhaa.

Soma zaidi: Serikali, upinzani Syria kuandika katiba mpya

Aidha kumekuwepo hasara kubwa ya mali japo hakukuwa na ripoti za majeruhi. Kulingana na shirika la habari la serikali SANA, shambulio hilo limetokea saa saba usiku wa kuamkia leo.

SANA imeripoti kuwa mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria ulizuia shambulio la Israel kwenye bandari ya Latakia japo makontena kadhaa yaliwaka moto katika shambulio hilo.

Picha na video zilizochapishwa na shirika hilo la habari zimeonyesha moto katika yadi ya kuhifadhi makontena japo baadaye likaripoti kuwa wazima moto walifanikiwa kuudhibiti moto huo.

Latakia ni mji wa bandari ulioko kaskazini mwa Syria, na upo umbali wa kilomita 230 kaskazini mwa Damascus. Chanzo kinachofahamu vizuri shughuli katika bandari ya Latakia, kimesema hii ni mara ya kwanza kwa Israel kufanya shambulio lililolenga bandari hiyo. Chanzo hicho kimesema bandari hiyo hutumiwa kwa kuingiza shehena ya silaha kutoka Iran.

Soma zaidi: Syria yatakiwa kutoa taarifa kuhusu silaza zake za sumu

Hata hivyo, ni nadra sana kwa Israel kuzungumzia juu ya mashambulizi ya anga inayofanya nchini Syria lakini mara kwa mara imesema haitoiruhusu Iran, ambaye ni adui wake mkubwa kujiimarisha zaidi na kuongeza ushawishi wake nchini Syria.

Tangu kuzuka kwa vita nchini Syria mnamo mwaka 2011, Israel imefanya mashambulizi ya anga chungu nzima katika ardhi ya Syria ikilenga vituo vya serikali pamoja na vikosi vya wapiganaji vinavyoungwa mkono na Iran pamoja na wapiganaji wa kundi la Hezbollah.

Iran imekuwa ikiiunga mkono serikali ya Syria katika mzozo huo uliodumu kwa muongo mmoja.