Israel yahimizwa kutojibu shambulizi la Iran
17 Aprili 2024Annalena Baerbock alikutana na mwenzake wa Israel, Israel Katz wakati wa ziara yake ambayo ni ya saba, tangu Hamas ilipovamia kusini mwa Israel Oktoba 7. Alikutana pia na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa mkuu wa upinzani nchini humo Benny Gantz, ambaye sasa ni mwanachama wa Baraza la mawaziri lenye jukumu la kusimamia vita. Katika mazungumzo yake na viongozi hao, Baerbock alijadili kwa kina hofu ya vita vinayoendelea katika Ukanda wa Gaza, kusambaa katika mataifa mengine na kuwa mzozo mkubwa wa kikanda.
Siku ya Jumamosi (13.04.2024), Iran ilirusha madroni na makombora nchini Israel kujibu shambulizi linalodaiwa kufanywa na Tel Aviv katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascu, Syria na Israel sasa imeapa kulipiza kisasi. Washirika wa Israel wanawasiwasi kwamba matukio kama haya, huenda yakasababisha mgogoro mkubwa katika eneo la Mashariki ya kati na kutaka kila mmoja kujizuwia.
Viongozi wa mataifa mbalimbali waiomba Israel na Iran kujizuia
Lakini David Cameron waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza, amesema ni wazi Israel imeamua kujibu shambulizi la Iran lakini anatumai jibu hilo litatekelezwa kwa njia ambayo haitotanua mzozo uliopo.
Kingine kinachotarajiwa kujadiliwa katika ziara hiyo ya Baerbock ni hali ya kibinaadamu ya watu wapalestina wanaoendelea kuteseka mjini Gaza ambako Israel inaendelea kushambulia huko, kwa lengo la kulitokomeza kundi ambalo nchi hiyo, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeliorodhesha kama kundi la kigaidi. Baerbock ametoa wito wa mara kwa mara kwa Israel kuidhinisha malori zaidi ya msaada kuingia katika ukanda huo.
Kundi la G7 latoa wito kwa Israel kutojibu shambulio la Iran
Kwengineko kundi la mawaziri wa nchi za nje wa nchi tajiri kiviwanda la G7, wanakutana kwa siku tatu mjini Capri Italia kujadili pamoja na mambo mengine vikwazo vipya dhidi ya Iran kufuatia shambulizi lake kwa Israel na msaada zaidi kwa Ukraine kuisaidia kupambana na uvamizi wa Urusi. Wakiongozwa na Italia inayoshikilia urais wa kupokezana wa kundi hilo la G7, viongozi hao wanatarajiwa kutoa tamko la pamoja na kuitaka Israel ijizuwiye kujibu mashambulizi.
UN: Vita vya Gaza vimewaathiri mno wanawake na watoto
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani, amesema amezungumza na mwenzake wa Israel, Israel Katz kuihimiza Israel kutotanua mgogoro na kufutilia mbali operesheni yake ya kijeshi inayotaka kufanya katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.
Huku hayo yakiarifiwa Umoja wa Mataifa umetoa wito wa bilioni 2.8 kutoa msaada wa dharura unaohitajika kwa wapalestina milioni 3 wanaokabiliwa na baa la njaa katika eneo linalokumbwa na vita la Gaza.
G7 yalaani shambulizi shambulizi la Iran dhidi ya Israel
Andrea De Domenico kutoka ofisi ya masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Gaza na Ukingo wa Magharibi, amesema juhudi kubwa zinahitajika ili watu wa Gaza waanze tena kupata huduma za matibabu, chakula na maji safi.
afp/ap/reuters