Israel yaizuia meli ya wanaharakati iliyokuwa inaelekea Gaza
4 Agosti 2018Idadi kubwa ya abiria 12 waliokuwamo katika meli hiyo wanatokea Sweden ingawa kuna wengine wanaotokea Ujerumani, UIngereza, Uhispania, Ufaransa na Canada. Msemaji wa mamlaka ya forodha ya Israel amesema watu hao wamezuiliwa kwa sasa ila watarudishwa makwao kwa ndege.
Mashua hiyo kwa jina SY Freedom for Gaza, ilikuwa imebeba dawa na vifaa vya matibabu tu na wawili kati ya abiria wake walikuwa wanahabari, amesema muandalizi wa anayetokea kikundi kimoja kinachoitwa Ship to Gaza ambacho kilipanga safari hiyo.
"Ship to Gaza inataka wale wote waliozuiliwa pamoja na meli na mizigo iliyokuwamo warudishwe katika eneo ambapo meli hiyo ilikuwa, na wakubaliwe waendelee na safari yao katika maji ya bahari ya Palestina bila kunyanyaswa, kulingana na sheria za kimataifa," limesema kundi hilo katika taarifa.
Jeshi la Israel liliwaelezea abiria kwamba wanakiuka amri
Israel inasema hatua ya wanamaji wake kuzuia meli kuingia Gaza inanuia kuzuia silaha kufikia makundi ya wanamgambo, likiwemo kundi la Hamas, ambalo ni vuguvugu la Kiislamu ambalo linadhibiti Palestina. Israel na Marekani wanalichukulia kundi la Hamas kama kundi la kigaidi.
"Jeshi la Israel limewaelezea abiria katika meli kwamba wanakwenda kinyume na amri ya jeshi ya kutoingia Gaza na kwamba bidhaa zozote za kiutu zinaweza kupelekwa Gaza kupitia bandari ya Israel na Ashdod," taarifa ya jeshi la Israel imesema.
Zaidi ya Wapalestina milioni 2 wako katika Ukanda wa Gaza ambao unakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Juhudi za Umoja wa Mataifa na Misri zinaendelea ili kutafuta suluhu la mzozo wa Israel na Hamas ambao wamepigana vita vitatu tangu mwaka 2008.
Maafisa wa Hamas hawakutoa tamko kuhusiana na kuzuiliwa kwa meli hiyo. Majaribio kama hayo ya wanaharakati kukiuka amri hiyo ya jeshi la Israel ya kuingia Gaza yametibuliwa. Tukio kubwa kama hilo lilikuwa mwaka 2010 pale makamanda wa Israel waliivamia meli ya Uturuki, Mavi Marmara, iliyokuwa inaongoza msururu wa mashua ndogo ndogo zilizokuwa zinaelekea Gaza. Wanaharakati 10 waliokuwa katika meli hiyo waliuwawa, jambo lililopelekea mzozo mkubwa wa kidiplomasia baina ya Uturuki na Israel.
Wakaazi 8,000 wa Gaza walikuwa wamekusanyika katika eneo la mpakani
Huku hayo yakiarifiwa kijana mmoja wa Kipalestina amefariki dunia Jumamosi kutokana na majeraha ya vidonda baada ya kupigwa risasi na majeshi ya Israel wakati wa mapambano katika mpaka wa Gaza, kulingana na wizara ya afya ya Ukanda huo iliyo chini ya uongozi wa Hamas.
Muadh al-Suri mwenye umri wa miaka 15 alipigwa risasi tumboni Ijumaa, amesema msemaji wa wiazara hiyo Ashraf al-Qudra na kupelekea idadi ya Waplestina waliouwawa na jeshi la Israel kwa kupigwa risasi kufikia watu 2, huku kukiwa na zaidi ya watu 200 waliojeruhiwa.
Kulingana na jeshi la Israel, karibu wakaazi 8,000 wa Gaza walikuwa wamekusanyika katika sehemu tofauti katika eneo hilo la mpakani, wakijaribu kuuharibu uzio wa mpakani wa Israel.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFP
Mhariri: Lilian Mtono