1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaongeza kasi ya mashambulizi Gaza

28 Juni 2024

Vikosi vya Israel vimeongeza kasi ya mashambulizi katika maeneo mawili ya kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4heGE
Israel-Yanga mbele kuelekea Rafah
Kifaru cha Israel na vikosi vya jeshi vyasogea karibu na mpaka na Ukanda wa Gaza.Picha: Amir Levy/Getty Images

Maafisa wa afya wa Palestina wakisema kuwa mashambulizi ya mizinga katika mji wa  Rafah yamewaua watu wasiopungua 11. 

Wakaazi na vyombo vya habari vya Hamas wameripoti kusonga mbele kwa vifaru upande wa magharibi katika kitongoji cha Shakoush, na kulazimisha maelfu ya watu waliohamishwa kuondoka kwenye kambi zao za mahema na kuelekea kaskazini hadi karibu na mji wa Khan Younis.

Soma pia: Wapalestina kadhaa wauawa katika mashambulizi Gaza

Kwa mujibu wa mkazi mmoja, baadhi ya tingatinga katika eneo la Shakoush zilikuwa zikirundika mchanga kwa pamoja ili vikosi vya Israeli vijifiche.

Israel pia imeripoti kufanya mashambulizi ya anga kaskazini mwa Gaza na kudai kuwaua "wanamgambo kadhaa” katika eneo la Shujaiya, pembezoni mwa mji wa Gaza ambalo limetajwa kuwa moja ya kamandi ya kundi za Hamas.

Haya yanajiri huku juhudi za upatanishi wa mataifa ya Kiarabu, zikiungwa mkono na Marekani, zikishindwa kupata makubaliano ya kusitisha mapigano hadi sasa. Hamas inasema mpango wowote lazima uwe wa kumaliza vita na kuitaka Israel kuondoa vikosi vyake kutoka Gaza, wakati Israel inasema itakubali tu kusitisha mapigano kwa muda hadi Hamas, ambayo imetawala Gaza tangu 2007, itakapotokomezwa.

Taka zarudikana karibu na kambi

Gaza | Nuseirat
Taka zimezagaa karibu na mahema kwenye kambi za waliokimbia makaazi yao katika Ukanda wa Gaza.Picha: AFP

Huku haya yakijiri takataka zinazooza zinarundikana karibu na mahema yanayoishi watu waliohama makaazi yao kote Gaza, huku maafisa wa Umoja wa Mataifa wakihofia kuenea kwa magonjwa kutokana na hali hiyo.

Akizungumza kutoka katikati mwa Gaza, afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Louise Waterridge ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatari ya kuibuka kwa maradhi ya kuambukizwa wakati karibu tani 100,000 za taka zikirundikana karibu na kambi kwenye ukanda wa Gaza.

Waterridge amesema joto kali la kiangazi, ukosefu wa vyoo, chakula na maji, huongeza athari ya kuzuka kwa magonjwa ya kuambukiza.

"Ni hali ngumu sana hapa kwa sasa kwa sababu ya joto la majira ya joto,  pia haya makazi wanayoishi watu yametenegenezwa kwa karatasi za plastiki kwa hiyo joto ndani ya karatasi la plastiki ni kubwa zaidi kuliko nje, halivumiliki na ngumu kuvumilia kuishi katika hali hizi."

Soma pia:Netanyahu: Israel inaelekea kukamilisha operesheni yake Gaza

Israel imekuwa ikitupa takataka katika sehemu nyingi za Ukanda wa Gaza mara baada ya shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7.