1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema imemuua kamanda wa Hezbollah ndani ya Lebanon

31 Julai 2024

Israel imefanya shambulizi la nadra jana jioni kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut, ambalo imesema limemuua kamanda wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah.

https://p.dw.com/p/4ivrt
Lebanon | Athari za shambulizi la Israel
Vifusi vya majengo viliporomoka kutokana na shambulizi la Israel mjini Beirut.Picha: ANWAR AMRO/AFP/Getty Images

Kamanda huyo anatuhumiwa kupanga shambulizi lililosababisha vifo vya vijana 12 kwenye eneo ambalo Israel inalikalia kwa mabavu la Milima ya Golan.

Israel iliapa kulipiza kisasi kwa shambulizi hilo la roketi la siku ya Jumamosi kwenye kitongoji cha Majdal Shams ikisema lilifanywa na  Hezbollah, madai ambayo kundi hilo imekuwa ikayakanusha.

Afisa mmoja wa Israel amesema shambulizi la mjini Beirut lilimlenga Fouad Shukur, kamanda wa ngazi ya juu wa Hezbollah ambaye amekuwa pia akitafutwa na Marekani kwa tuhuma za kupanga na kutekeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake mnamo 1983.

Shukur pia anadaiwa kuhusika na mashambulizi mengine yaliyowaua raia wa Israel.

Shirika la Habari la Lebanon limeripoti shambulizi la mjini Beirut lilifanywa kwa kutumia droni iliyofyetua makombora matatu.

Inaarifiwa limetokea kwenye eneo la kusini mwa mji huo mkuu wa Lebanon liitwalo Haret Hreik. Ni eneo ambalo limefurika watu ambako kundi la Hezbollah huendesha operesheni zake za kisiasa na kijeshi.

Wizara ya Afya ya Lebanon imesema kwenye shambulio hilo mwanamke mmoja na watoto wawili wameuwawa na watu wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa.

Israel yasema Hezbollah "ilivuka mstari mwekundu", kundi hilo laahidi kulipa kisasi 

Lebanon | Shambulizi la Israel mjini Beirut.
Sehemu ya majengo yaliyopata athari kutokana na shambulizi la Israel mjini Beirut.Picha: Ahmad Al-Kerdi/REUTERS

Muda mfupi baada ya shambulizi la mjini Beirut kuripotiwa waziri wake wa ulinzi Yoav  Gallant aliandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X kwamba "Hezbollah ilivuka mstari mwekundu."

Waziri Mkuu wa mpito wa Lebanon Najib Mikati amelaani shambulio hilo la Israel akisema lilipiga mita chache kutoka moja ya hospitali kubwa kabisa za mji huo mkuu.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hakutoa taarifa yoyote ya haraka lakini dakika chache baada ya shambulizi hilo ilichapisha picha ya Netanyahu akiwa pamoja na mshauri wake wa masuala ya usalama na maafisa wengine.

Kwa upande wake Hezbollah nayo imesema italipa kisasi.

"Israel imefanya kitendo cha kijinga kwa ukubwa wake, muda iliyochagua na mazingira kwa kulilenga eneo zima la maakazi ya raia," amesema Ali Ammar, afisa wa kundi la Hezbollah alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Al-Manar. "Israel italipa kwa haya hivi karibuni au baadaye."

Shambulizi hilo la Israel limeitumbukiza kanda ya mashariki ya kati kwenye ukingo wa vita vipana. Pande hizo mbili zimekuwa zikishambulia karibu kila siku kwa miezi 10 iliyopita tangu kuanza kwa vita vya Gaza lakini kila upande ulijizuia kuutanua mvutano wao.

Hata hivyo baada ya hujuma ya siku ya Jumamosi kwenye milima ya Golan, Israel ilisema ingejibu vikali dhidi ya kundi la Hezbollah kufuatia mkasa wa Jumamosi.