Israel yasema 'shambulizi la Iran litajibiwa'
16 Aprili 2024Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliongoza kikao cha baraza la vita la serikali yake jana usiku ambacho kilidumu kwa saa tatu na kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa kujibu shambulizi hilo la Iran. Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha Channel 12 cha nchini humo, hatua zilizojadiliwa na baraza hilo la mawaziri la vita zilianzia kwa zile ndogo hadi zile kali zaidi. Kiliripoti kuwa Israel inalenga kuweka usawa kati ya kusababisha uharibifu nchini Iran lakini sio kuzusha vita vya kikanda. Mshirika mkuu wa Israel, Marekani, ilisema haifahamu mipango yoyote.
Soma pia: Viongozi wa dunia waihimiza Israel kutolipiza kisasi
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameitaka Israel kuchangia hatua zitakazotuliza mzozo katika kanda hiyo ya Mashariki ya Kati licha ya shambulizi la Iran dhidi yake. Kansela Scholz amewaambia waandishi wa habari mjini Shanghai, China kwamba vilevile Iran lazima ikomeshe uchokozi. Ujerumani ilimuita balozi wa Iran mjini Berlin kufuatia shamubulizi hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amekiambia kituo cha Utangazaji cha BBC kwamba kwamba Uingereza haiungi mkono ulipizaji kisasi.
Baadhi ya serikali za Afrika nazo zimezihimiza Israel na Iran kuepusha kuchochea mgogoro zaidi.