1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia maeneo ya karibu na Damascus

26 Desemba 2018

Inadaiwa kuwa ndege za kivita za Israel zimefyatua makombora kuelekea maeneo ya karibu na mji mkuu wa Syria Damascus jana usiku, na kulipiga ghala la silaha na kuwajeruhi wanajeshi watatu

https://p.dw.com/p/3AdVP
Syrien Staatsmedien: Syrische Luftabwehr reagiert auf Angriff nahe Damaskus
Picha: picture-alliance/Xinhua/A. Safarjalani

 Shirika la habari la Lebanon liliripoti kuwa ndege za kivita za Israel ziliruka katika anga ya kusini mwa Lebanon. Shirika la haki za binaadamu la Syria limesema mashambulizi ya angani ya Israel yaliyalenga maeneo matatu kusini mwa Damascus ambayo ni maghala ya silaha ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon na wanajeshi wa Iran.

Shambulizi hilo ni la kwanza tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipotangaza wiki iliyopita kuwa Marekani itawaondoa wanajeshi wake wote 2,000 nchini Syria, hatua ambayo itaacha wazi udhibiti wa upande wa mashariki mwa Syria wenye utajiri wa mafuta. Hakujawa na taarifa yoyote kutoka kwa jeshi la Israel kuhusu shambulizi nchini Syria.

Russland Raketenabwehrsystem S-300
Mfumo wa ulinzi wa anga aina ya S-300Picha: picture alliance/dpa/TASS/S. Bobylev

Mashambulizi hayo yanayoshukiwa kufanywa na Israel yamekuja siku mbili baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusema kuwa kuondolewa kwa wanajeshi 2,000 wa Marekani kutoka kaskazini mashariki mwa Syria hakutoibadili sera ya Israel ya kuwalenga wanajeshi wa Iran nchini Syria. "Tutaendelea kuchukua hatua dhidi ya jaribio la Iran kuwa na uwepo wake kijeshi nchini Syria, na kama patakuwa na haja, tutatanua shughuli zetu nchini humo". Alisema Netanyahu.

Israel imekuwa ikifanya mashambulizi kadhaa ya angani katika maeneo yanayoshukiwa kuwa ya jeshi la Iran na wapiganaji wa Hezbollah nchini Syria, ambako wanaunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Hata hivyo, Israel imewekewa kizuizi cha kufanya mashambulizi nchini Syria tangu Oktoba wakati Urusi iliipa Syria mfumo wa ulinzi wa anga aina ya S-300 ambao unayaharibu makombora yanayofyatuliwa na adui. Hilo lilijiri mnamo Septemba 17 wakati ndege ya kijeshi ya Urusi ilipoangushwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria wakati wa shambulizi lililofanywa na Israel.

Tukio hilo lilizusha mvutano kati ya Urusi na Israel, ambazo kawaida huwa na mahusiano mazuri na zina kiwango fulani cha ufahamu kuhusu Syria. Mashambulizi ya anga ya Israel yanachukuliwa na Urusi kuwa yanayoweza kuiyumbisha Syria ambako Urusi inalenga kuuyalinda mafanikio ambayo utawala wa Assad umepata katika vita vya vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. wakati huo huo, wachambuzi wanasema Urusi inafahamu wasiwasi wa usalama ambao Israel iko nao kuhusu mpango wa Iran wa urutubishaji wa madini ya urani

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters/AP