1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel imethibitisha kukishambulia kivuko cha mpakani

Angela Mdungu
25 Oktoba 2024

Jeshi la Israel limethibitisha kukishambulia kivuko cha mpakani baina ya Syria na Lebanon, ilichosema kinatumiwa na wanamgambo wa Hezbollah kusafirisha silaha.

https://p.dw.com/p/4mEm6
Helikopta ya Israel yarusha kombora kusini mwa Lebanon
Helikopta ya Israel yarusha kombora kusini mwa LebanonPicha: Leo Correa/AP Photo/dpa/picture alliance

Jeshi hilo limeongeza kuwa mashambulizi yake ya anga yameilenga miundombinu kwenye kivuko cha Jousieh kilichoko katika eneo la Bekaa kaskazini mwa Lebanon usiku wa kuamkia Ijumaa. Limesema Hezbollah inakitumia vibaya kivuko hicho cha raia, ambacho kiko chini ya udhibiti wa utawala wa Syria na kinaendeshwa na usalama wa kijeshi wa nchi hiyo. Kivuko hicho kinachofahamika kama Qaa upande wa Lebanon ni cha pili kushambuliwa na jeshi la Israel ndani ya mwezi huu. Israel inasema mashambulizi yake yanalenga kuzuia uingizaji wa silaha nchini Lebanon hadi mikononi mwa Hezbollah inayoungwa mkono na Iran kutoka nchi jirani ya Syria.