1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yauachia msafara wa wafanyakazi wa UNRWA Gaza

10 Septemba 2024

Msafara wa magari na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa uliokamatwa na Israel kaskazini mwa Ukanda wa Gaza umeachiwa huru saa nane tangu ulipowekwa chini kizuizi cha maafisa wa usalama.

https://p.dw.com/p/4kRVY
GAZA | Usambazaji chanjo ya polio
Mkuu wa shirika la UNRWA amesema msafara uliozuiwa ulikuwa unasambaza chanjo dhidi ya Polio. Picha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Taarifa hizo zimetolewa na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa KIpalestina, UNRWA. Jeshi la Israel lilisema jana Jumatatu kwamba liliuzuia msafara huo baada ya kupokea taarifa za kiintelejensia kwamba "watuhumiwa kadhaa wa Kipalestina" walikuwemo ndani ya magari na ilitaka kuwahoji.

Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini amesema msafara huo uliwekwa chini ya mtutu wa bunduki huku kukitolewa vitisho vya kukamatwa kwa wafanyakazi waliokuwemo.

Amesema pia magari ya shirika hilo yameharibiwa na matingatinga ya Israel kabla ya wanajeshi kuuruhusu kuondoka na wafanyakazi wote waliokuwemo wamerejea salama katika kambi ya Umoja wa Mataifa.

Lazzarini amesema msafara huo ulikuwa unakwenda kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kaskazini mwa Gaza na kwamba hana uhakika iwapo zoezi hilo litaendelea tena leo Jumanne.