1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaushambulia mji wa Rafah

9 Februari 2024

Israel imeushambulia mji wa Rafah ulioko kusini mwa Gaza leo, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kusema hatua za Israel zimepitiliza katika kujibu mashambulio ya Hamas ya Oktoba 7.

https://p.dw.com/p/4cETj
Matokeo ya mashambulizi ya Israel kwenye eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Matokeo ya mashambulizi ya Israel kwenye eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/picture alliance

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema amewaamuru wanajeshi wa Israel kujiandaa kwa operesheni katika mji wa Rafah, mji wa mwisho mkubwa katika Ukanda wa Gaza, ambao bado haujavamiwa na majeshi ya ardhini ya Israel.

Marekani ndiyo mshirika mkuu wa kimataifa wa Israel, ikiipatia nchi hiyo mabilioni ya dola katika msaada wa kijeshi.

Soma zaidi: Biden: Operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza imepitiliza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema haiungi mkono mashambulizi ya ardhini mjini Rafah, na kuonya kuwa ikiwa haijapangiliwa vyema, operesheni kama hiyo katika mji unaowahifadhi Wapalestina zaidi ya milioni moja waliohama makaazi yao inahatarisha kusababisha "janga."

Katika karipio lisilo la kawaida, Biden alisema hatua za kijeshi Gaza zimepitiliza na kutaka zikomeshwe.