Israel yaushambulia Ukanda wa Gaza
13 Machi 2014Wapalestina walioshuhudia, pamoja na mpigaji picha wa shirika la habari la AFP wamesema ndege za kivita zilizishambulia kambi za watawala wa chama cha Hamas na kitengo cha kijeshi cha kundi la Islamic Jihad, Al-Quds Brigades, ambalo limedai kuhusika na mashambulizi hayo.
Taarifa ya jeshi la Israel imesema siku ya Jumatano usiku kwamba mabaki ya maroketi 60 yamepatikana, matano kati ya hayo yakisemekana kuanguka katika maeneo yenye watu wengi. Ripoti hiyo imemnukuu luteni kanali Peter Lerner akisema operesheni hiyo imefanyika kwa umakini mkubwa na bila kuchelewa. "Tumeilenga miundombinu inayowasaidia magaidi wakati wanapopata mafunzo, kupanga na kutekeleza mashambulizi yao. Hawataruhusiwa kupanga njama katika usalama wa mahekalu ya magaidi," ikaendelea kusema ripoti hiyo.
Wapiganaji wa Al-Quds Brigades wamesema wamefyetua maroketi 90 nchini Israel kulipiza kisasi mauaji ya wenzao watatu waliouwawa siku ya Jumanne kusini mwa Gaza katika shambulizi la angani la jeshi la Israel. Wapiganaji hao wametoa tamko wakisema mashambulizi yao yataendelea kujibu hujuma ya Israel ya Jumanne wiki hii. Hamas imeionya Israel dhidi ya kuchochea makabiliano.
Miito yatolewa kuepusha machafuko
Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, ametoa taarifa kupitia msemaji wake akihimiza kile alichokiita uchochezi wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza ukome.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameyalaani vikali mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel na kutoa mwito pande zote mbili zijizuie ili kuepusha machafuko zaidi yanayoweza kuliyumbisha eneo hilo. Mjini Washington msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki, katika taarifa yake amesema mashambulizi hayo dhidi ya Israel hayana uhalali na ametoa mwito yakome mara moja.
Mashambulizi hayo yaliyosababisha taharuki miongoni mwa maelfu ya Waisraeli wa kusini na kuwalazimu kutafuta hifadhi, yanaelezwa kuwa wimbi makubwa zaidi tangu vita vya siku nane vya Novemba 2012 kati ya Israel na Hamas. Operesheni hiyo ya Israel dhidi ya Gaza iliyopewa jina "Pillar of Defence" yaani Ngao ya Ulinzi, ilisababisha vifo vya wanajeshi sita wa Israel na Wapalestina 177, wengi wao wakiwa raia. Hakukuwa na taarifa zozote na majeruhi kutoka pande zote mbili.
Duru za usalama za Gaza zinasema wafanyakazi wa utawala wa Hamas, wakiwemo maafisa wa kitengo cha kijeshi cha kundi hilo, Ezzedine Al-Qassam Brigades, walikuwa awali wameondoka kambini mwao kabla Israel kushambulia.
Netanyahu aja juu
Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, kufanya ziara yake ya kwanza katika eneo hilo tangu alipoingia madarakani mwaka 2010. Yalianza muda mfupi baada ya Cameron na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kulihutubia bunge.
Katika tamko lililotolewa na ofisi yake Netanyahu, ameonya atachukua hatua kali na kuwaonya wanamgambo wa Gaza akisema, "Kama hakutakuwa na kimya kusini mwa Israel, basi kutakuwa na kelele Gaza." Taarifa hiyo imesema Netanyahu amekutana na wakuu wa usalama na ulinzi na kuwaagiza wachukue hatua zozote kurejesha utulivu.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, waziri wa ulinzi wa Israel, Moshe Yaalon ameamuru kivuko cha Kerem Shalom kinachotumiwa kupitishia bidhaa kati ya Israel na Gaza na kivuko cha Erez ambacho kinatumiwa na watu vifungwe mpaka hali ya usalama itakapotathminiwa upya.
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Israel, Avigdor Lieberman amesema Israel haitakuwa na chaguo lengine ila kuukalia tena Ukanda wa Gaza ambao iliuhama wakati wa msimu wa kiangazi mwaka 2005.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE/DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba