1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawakataza raia wake kuzuru Uturuki

17 Mei 2018

Waziri wa utalii wa Israeli Yariv Levin amewataka raia wa Israel wasisafiri kwenda Uturuki wakati ambapouhusiano wa kidiplomasia kati ya hizo mbili ukizidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/2xtnY
Symbolbild Türkei plant neuen Kanal neben Bosporus in diesem Jahr
Picha: picture alliance/prisma

Uturuki ni sehemu ambayo inapendelewa zaidi na watalii kutoka Israel. Takriban watalii 380,000 raia wa Israeli waliitembelea Uturuki mwaka jana wa 2017, hayo ni kulingana na takwimu rasmi za nchini Uturuki. Uturuki na Israel zimekuwa na uhusiano mbaya katika miaka ya hivi karibuni, na hali hiyo imeongezeka hasa baada ya Wapalestina 60 kuuawa na wanajeshi wa Israel katika eneo la mpaka kati ya Ukanda wa Gaza na Israel wakati walipoandamana.

Eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza lashambuliwa

Mapema leo jeshi la Israel lilifanya mashambulizi katika eneo la kaskazini mwa ukanda wa Gaza ambapo Israel imesema hiyo ilikuwa ni hatua ya kujibu mashambulizi ya Hamas kuelekea mji wa Israel wa Sderot, ulioko mpakani. waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake itaendelea kujilinda dhidi ya kundi la Hamas.

Kwa upande mwengine Mahakama moja nchini Israel imelikataa ombi la Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, la kutaka kufukuzwa kwa mwakilishi wake nchini Israel kucheleweshwe, hadi pale kesi ya rufaa dhidi ya kufukuzwa kwake itakaposikilizwa. Mwakilishi huyo, Omar Shakir ambaye ni raia wa Marekani, na anayedaiwa kuikosoa Israel, amebakiwa na muda wa wiki moja kuwa amefungasha na kuondoka. Afisa huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jaji amempa hadi tarehe 24 Mei kuwa ameondoka.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Wakati huo huo katika tukio jengine linalohusiana na hali ya mambo huko Mashariki ya Kati, waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameikemea kupitia kwenye ukurasa wake wa Twitter hatua ya Marekani na Saudi Arabia ya kuwawekea vikwazo washirika wake nchini Lebanon ambao ni viongozi wa kundi la Hezbollah. Javad Zarif amesema hatua hiyo ya Saudi Arabia na mshirika wake Marekani hasa wakati ambapo mwezi mtukufu wa Ramadhan umeanza ni aibu.

Hezbollah yawekewa vikwazo

Marekani na nchi sita za Ghuba zimetangaza vikwazo dhidi ya uongozi wa Hezbollah, huku Marekani ikiwa na nia ya kuimarisha shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran na washirika wake katika kanda ya Mashariki ya kati baada ya Rais Donald Trump kuiondoa nchi yake kutoka kwenye mpango wa nyuklia wa Iran uliofikiwa mwaka 2015. Umoja wa Ulaya umeiweka Hezbollah kwenye orodha ya makundi ya kigaidi tangu mwaka 2013.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/DPA/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman