1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yazingira hospitali mbili zaidi mjini Khan Younis

Sylvia Mwehozi
25 Machi 2024

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema kuwa vikosi vya Israel vilizingira hospitali mbili mjini Gaza na kuzuia timu ya madaktari chini ya milio mikali ya risasi huku Israel ikidai kuwakamata wanamgambo 480.

https://p.dw.com/p/4e5WQ
Al Shifa-Gaza
Askari wa Israel wakiwa wanalinda doria hospitali ya Al ShifaPicha: Ronen Zvulun/Reuters

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema kuwa vikosi vya Israel vilizingira hospitali mbili mjini Gaza na kuzuia timu ya madaktari chini ya milio mikali ya risasi huku Israel ikidai kuwakamata wanamgambo 480.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, inasema kuwa mmoja wa wafanyakazi wake ameuawa wakati vifaru vya Israel vilipovamia maeneo ya karibu na hospitali za Al-Amal na Nasser katika mji wa kusini wa Khan Younis, huku kukiwa na mashambulizi ya mabomu na milio ya risasi.Hamas yasema waliokufa tangu kuanza kwa vita ni 32,142

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, ni kwamba vikosi vyake vilishambulia maeneo ya karibu na hospitali ya Al-Amal kufuatia "taarifa za kijasusi zilizoashiria kwamba magaidi wanatumia miundombinu ya kiraia kufanya shughuli za kigaidi katika maeneo hayo".

Khan Younis -Hospitali ya Nasser
Hospitali ya Nasser mjini Khan YounisPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limeongeza kwamba vikosi vya Israel hivi sasa vinataka kuondoka kabisa kwa wafanyakazi, wagonjwa na watu waliokimbia mapigano kutoka viunga vya hospitali hiyo na vilikuwa vikirusha mabomu katika eneo hilo ili kuwalazimisha watu kuondoka. Kulingana na shirika hilo, Mpalestina mmoja ameuawa ndani ya maeneo ya hospitali.

Soma: Gaza yapigwa mabomu huku UN ikisisitiza upelekwaji msaada

Nayo wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, ilisema kuwa wagonjwa takribani 12 na wafanyakazi wa matibabu wanashikiliwa na vikosi vya Israel katika hospitali ya Al Shifa iliyoko upande wa Kaskazini ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa Israel kwa wiki sasa. Ofisi ya mawasiliano ya serikali inayoendeshwa na Hamas pia imesema madaktari watano wameuawa na vikosi vya Israel katika kipindi cha wiki moja cha operesheni yake katika hospitali ya Al Shifa.

Wakati Gaza ikiendelea kuandamwa na mashambulizi ya anga na mizinga ya Israel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ametoa wito wa kuongezwa kwa usambazaji wa misaada katika ukanda huo uliozingirwa aliosema umegubikwa na "hofu na njaa". Ameongeza kwamba "tunaongeza shinikizo zaidi kadri  tuwezavyo ili kufikia usitishaji mapigano wa kibinadamu, kuruhusu kukomesha umwagaji damu na kuruhusu ufikiaji wa misaada ya kiutu kwa watu wote wa Gaza ambao wanakabiliwa na njaa".

Viongozi wengine wa dunia nao wameungana na Guterres katika kutoa wito wa usitishaji haraka wa vita na kuitaka Israel pia kusimamisha mipango yake ya kutuma wanajeshi wake katika mji wa kusini wa Rafah.

Khan Younis | Wagonjwa hospitalini Nasser
Wapalestina waliojeruhiwa katika hospitali ya Nasser Picha: AHMED ZAKOT/REUTERS

Huko jijini New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa hii leo kulipigia kura azimio jipya linalotaka usitishaji wa "haraka" wa vita Gaza, baada ya Urusi na China kulipinga azimio lililopita la Marekani. Tangu mzozo huo uanze, Baraza la Usalama limegawanyika ambapo ni maazimio mawili kati ya manane yaliyoidhinishwa ambayo yalihusu misaada ya kiutu katika Ukanda huo.

Azimio hilo jipya ambalo limeonwa na shirika la habari la AFP, "linataka usitishwaji wa haraka" wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaoendelea, na kupisha njia ya kuelekea "usitishaji kamili na endelevu".

Azimio hilo limeandaliwa na wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama. China tayari imesema kwamba italiunga mkono azimio hilo jipya.