Israeli imefyatua risasi kwenye hadhara ya Wapalestina
27 Aprili 2018Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu amesema kuwa Israel imetumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji eneo hilo katika siku za hivi karibuni.
Kiasi ya Wapalestina 40 wameuawa kwa kupigwa risasi na Waisrali kwenye mpaka tangu mpango wa majuma sita wa maandamano ulioanza Machi, 30 huku kukikosekana majeruhi upande wa Israeli. Idadi ya waandamanaji huongezeka na kufika maelfu baada ya swala ya Ijumaa.
Maafisa wa matibabu wa Palestina walisema kuwa yumkini vijana watatu walijeruhiwa kwenye tukio hilo karibu na kambi ya mahema kwenye mpaka wa Gaza-Israel, huku waandamanaji wengine wakirusha mawe na kubingirisha matairi kwenye sengénge iliyoko mpakani.
Kwenye taarifa iliyotolewa mapema Ijumaa, mkuu wa Umoja wa mataifa anayesimamia masuala ya haki za bindamu Zeid Ra'ad al-Hussein alitaja kuangamia kwa maisha "kuwa ya kusikitisha" na na idadi ya majeruhi ilisababishwa na mtutu wa risasi.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel haikutoa taarifa mara moja, lakini mara kwa mara serikali imesema kuwa inalinda mipaka yake na kwamba jeshi lake linazingatia utaratibu wa sheria.
Kilele cha maandamano ni Mei, 15
Maandamano hayo makubwa yaliyopewa jina, 'Msafara mkubwa wa kurejea', yanafufua shuruti kubwa la haki ya Wapalestina walioko kwenye kambi za wakimbizi kurejea mijini na vijijini. Wakimbizi hao walitoroka au kutoroshwa pamoja na familia zao wakati taifa la Israel lilipoundwa mwaka 1948.
Hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa mahema kwenye kambi katika eneo ambalo Isarel hairuhusu watu kufika, kilomita 40 katika mpaka wake. Kilele cha maandamano hayo ni tarehe 15 mwezi Mei wakati Wapalestina wanaadhimisha siku kuu ya Nakba, ama siku ya Majanga, kukumbuka miaka 70 iliyopita ambapo walipoteza makazi yao.
Israel iliondoa wanajeshi wake na walowezi kutoka Gaza mwaka 2005 lakini inadhibiti mipaka ya kipande chake cha ardhi na bahari.
Wapalestina 42 wameuawa na wanajeshi wa Israeli tangu mwezi Machi 30, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Wengi wa waandamanaji Wakipalestina waliouawa na Israel tangu kuanza kwa "Msafara mkubwa wa Kurejea" walipigwa risasi kenye mpaka huku wachache wakiuawa katika mashambulio ya angani.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman