1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISTANBUL: Mauaji ya mwandishi wa habari nchini Uturuki yasababisha shutuma za kimataifa.

20 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCZM

Mauaji ya mwandishi wa habari mturuki Hrant Dink mwenye asili ya Armenia yamesababisha shutuma kali katika maeneo kadhaa duniani.

Ujerumani, inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya, imeelezea kufadhaishwa na mauaji hayo.

Maelfu ya watu wameandamana baada ya mtu asiyejulikana kumpiga risasi na kumuua mwandishi huyo wa habari nje ya afisi ya gazeti alilokuwa akifanyia kazi.

Duru zinasema polisi wa Uturuki wanawahoji watu kadhaa kuhusu tukio hilo.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wakuu wa serikali ya Armenia wameitwika lawama serikali ya Uturuki kwa kukosa kumwekea ulinzi Hrant Dink ingawa alikuwa amearifu kuwa maisha yake yalikuwa hatarani.

Hrant Dink aliingia matatani kwanza kwa maoni yake yaliyozua hasira kuhusu mauaji ya raia wa Kiarmenia waliouawa kati ya mwaka elfu moja mia tisa na kumi na tano na mwaka elfu moja mia tisa na kumi na nane nchini Uturuki.

Mwaka uliopita Hrant Dink alitengewa kifungo cha miezi sita kwa kuvunja sheria alipotoa matamshi yaliyosemekana yaliudharau utaifa wa Uturuki.

Hrant Dink atazikwa siku ya Jumanne ijayo.