ISTANBUL : Mwandishi wa Kituruki auwawa
20 Januari 2007Mjini Instanbul mamia ya watu wameandamana kulaani mauaji ya Hrant Dink mwandishi wa habari wa Kituruki mwenye asili ya Armenia.
Mhariri huyo wa gazeti alipigwa risasi nje ya makao makuu ya gazeti lake. Dink aliamsha hasira za utaifa kutokana na maoni yake juu ya mauaji ya umma wa Warmenia yaliofanywa na Himaya ya Waturuki kati ya mwaka 1915 na mwaka 1918 ambayo ameyaita kuwa ni mauaji ya kimbari.
Mwaka jana mwandishi huyo alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita kwa kuvunja sheria tata dhidi ya kuutukana Uturuki.
Waziri Mkuu Recep Erdogan kwa haraka amelaani mauaji hayo na kuyaita kuwa ni shambulio dhidi ya uhuru wa maoni. Waandishi wa habari na wanasiasa nchini Uturuki wameelezea kukasirishwa kwao na mauaji hayo ambapo wengi wanayaeleza kuwa ni mauaji ya kisiasa wakati Marekani,Umoja wa Ulaya na Armenia pamoja na makundi kadhaa ya kutetea haki za binaadamu pia zikielezea kufadhaishwa kwao na kuyalaani mauaji hayo.
Serikali ya Uturuki imesema imewakamata watu watatu kuhusiana na mauaji hayo.