ISTANBUL : Papa akamilisha ziara yake Uturuki
1 Desemba 2006Ziara ya Papa Benedikt wa 16 nchini Uturuki inamalizika leo hii na inaonekana kuwa kama ya mafanikio makubwa kwa jitihada zake za kurekebisha uhusiano ulioathirika na Waislamu wa Uturuki.
Benedikt aliwakasirisha Waislamu wengi hapo mwezi wa Septemba kwa hotuba yake ilioihusisha dini ya Uislamu na matumizi ya nguvu lakini alipongezwa na Uturuki wakati alipowasili hapo Jumanne kwa kuunga mkono harakati za Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya na kuisifu dini ya Kiislam kuwa ni dini ya amani.
Hapo jana alizuru msikiti kwa mara yake ya kwanza akiandamana na Mufti Mkuu wa Istanbul Mustafa Cagrici ambapo waliomba Mungu kwa pamoja kwenye Msikiti Buluu ambao ni mashuhuri kabisa mjini Istanbul.Mtangulizi wa Benedikt Papa John Paul alikuwa ni papa wa kwanza kuzuru msikiti mjini Damascus Syria hapo mwaka 2001.
Katika ziara yake ya Uturuki Papa Benedikt pia alikuwa na mazungumzo na Askofu Mkuu Batholomeu wa Kwanza wa Wakiristo wa madhehebu ya Orhodox ambapo wamesema haki za makabila ya watu wachache lazima zilindwe wakati Umoja wa Ulaya ukitanuka.