1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia: Juhudi za kupambana na Corona zaendelea

Angela Mdungu
25 Februari 2020

Idadi ya vifo kutokana na virusi vya Corona imeendelea kuripotiwa katika mataifa mbalimbali duniani. Italia ambayo imeshuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo imeitisha mkutano kukabiliana na virusi hivyo

https://p.dw.com/p/3YN5q
Iran Coronavirus Vorsichtsmaßnahme
Picha: Reuters/Wana News Agency/N. Tabatabaee

Italia iliripoti siku ya jumatatu kuwa, vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya Corona  nchini humo imefikia watu saba na kuna zaidi ya visa 220 vya watu walioambukizwa. Maambukizi yameripotiwa zaidi katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na miji jirani ya Lombardy na Veneto.  Nazo taarifa  za wizara ya afya ya Uhispania zinasema watalii katika moja ya hoteli na wafanyakazi katika visiwa vya Kanari nchini humo wamezuiliwa na wanafanyiwa vipimo kujua  iwapo wamepata maambukizi ya virusi hivyo.

Hayo yanajiri wakati  Italia ikitarajiwa kuongoza mkutano utakaowahusisha mawaziri wa afya toka nchi jirani ili kujadili na kuwa na utaratibu wa kukabiliana na viruzi hivyo Kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa wizara ya afya ya nchi hiyo, mawaziri watakaoshiriki kwenye mkutano huo  ni wa kutoka Austria, Ufaransa, Slovenia Uswisi, Ujerumani na Croatia.

Juhudi hizo za kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo zinaendelea huku Iran nayo ikiripoti kuwa watu 12 wamefariki kutokana na maambukizi ya Corona. Hata hivyo idadi hiyo inakinzana na mbunge wa jimbo la Qom yalipoanzia maambukizi nchini humo Amirabadi Farahani, aliyedai kupitia shirika moja la habari nchini humo kuwa watu waliofariki kutokana na virusi hivyo ni 50.

Ausbruch des Corona-Virus im Iran 2020
Baadhi ya raia wa Iran wakiwa wamevaa barakoa kujikinga na virusi vya CoronaPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/R. Fouladi

Kwa upande wake China vilipoanzia virusi hivyo imeripoti  vifo vipya 71 ambapo 68 kati ya hivyo ni kutoka katika mji wa Wuhan vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza virusi hivyo.  Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumzia mambukizi ya virusi hivyo ametoa wito kwa mataifa kufanya kila namna kabiliana na janga hilo.

Kando ya China, Iran na Italia, baadhi ya nchi zilizoripoti pia kuwa na maambukizi ya virusi pamoja na Japan ambako vyombo vya habari vimeripoti vifo vinne baada ya waathiriwa kupata maambukizi wakiwa katika meli ya kifahari ya  Diamond Princess iliyowekwa karantini kwa wiki mbili katika bandari nchini humo. Nchi nyingine zilizoripoti pia kuwa na maambukizi hivi karibuni, ni pamoja na Iraq, Japan, Kuwait, Afghanistan Oman na badhi ya mataifa ya Ulaya.