Italia na Brazil kuumana katika dimba la wanawake
18 Juni 2019Hali hiyo itajitokeza wakati itakapokumbana na Brazil katika mpambano ambao unarejesha kumbukumbu za zamani za kombe la dunia kwa wanaume. Nigeria ilifungwa bao 1-0 na Ufaransa, lakini ikiwa katika nafasi ya tatu katika kundi lao A inasubiri kuona iwapo inaweza kupenya katika timu 16 zinazosalia ili kuingia katika awamu ya mtoano.
Italia ina pointi sita baada ya kufunga mabao saba katika michezo yake miwili ya ufunguzi , ikiwa ni pamoja na ushindi wa kushitua dhidi ya timu iliyopigiwa upatu kufanya vizuri kabla ya mashindano hayo Australiam, na inahitaji sare tu dhidi ya Brazil kujihakikishia kuwa vinara wa kundi C.
Pambano hiyo linazusha kumbukumbu ya fainali za wanaume katika kombe la dunia, ikiwa ni pamoja na kichapo kilichotayarishwa kupitia Pele enzi hizo cha mabao 4-1 dhidi ya Italia katika fainali ya mwaka 1970 na mabao matatu ya Paolo Rossi mwaka 1981, ambayo yalikizamisha kikosi kilichokuwa kinaongozwa na Zico na hatimaye Italia kutoroka na taji hilo.
Australia inaweza kunyakua nafasi ya pili iwapo wataishinda Jamaica, ambao wameshindwa kupata bao wakati wakipoteza michezo yao yote, na Brazil kushindwa kupata ushindi.
Ufaransa vinara kundi A
Norway inawasubiri viongozi wa kundi C katika awamu ya timu 16 zitakazobaki baada ya kikosi cha kocha Martin Sjogren kuwapiku Korea kusini kwa mabao 2-1 mjini Reims jana Jumatatu, na kumaliza wapili katika kundi A.
Ufaransa imejihakikishia kuwa vinara wa kundi A baada ya kupata bao moja tu katika mchezo wake dhidi ya Nigeria, bao lililofungwa kutokana na mkwaju wa penalti ambayo ilibidi kurudiwa mjini Rennes.
Ufaransa inakabiliwa na uwezekano wa pambano la robo fainali dhidi ya mabingwa watetezi Marekani iwapo Marekani itakuwa vinara wa kundi F na kuingia katika timu 16 kama inavyotarajiwa.
Ujerumani imehakikisha kwamba inaikwepa Marekani katika awamu ijayo baada ya kuirarua Afrika kusini kwa mabao 4-0 na kumaliza ikiwa kileleni mwa kundi B.
Uhispania inauwezekano wa kutiana kifuani an Marekani baada ya kumaliza ikiwa ya pili katika kundi B nyuma ya Ujerumani baada ya kutoka sare bila kufungana na China ambao pia wanahakika ya kuendelea na mashindano hayo kama timu bora ya tatu.