Jaji anayechunguza mauaji ya rais wa Haiti ajitowa
14 Agosti 2021Jaji Mathieu Chanlatte aliyeteuliwa wiki iliyopita, alitangaza uamuzi wake kwenye barua aliyomuandikia mkuu wa mahakama ya mwanzo, Benard Saint-Vil, siku ya Ijumaa (13 Agosti).
"Tunajiondowa kwenye kesi hii kwa sababu za kibinafsi na tunaamuru kurejwa kwa mkuu wa mahakama hii," alisema Jaji Chanlatte kupitia barua aliyoamuandikia Saint-Vil.
Saint-Vil aliliambia shirika la habari la AP kwamba angechaguwa jaji mwengine wa kuchukuwa nafasi ya Chanlatte ndani ya siku chache zijazo.
Licha ya kutokuelezea undani wa sababu za kujiuzulu, uamuzi huo wa Chanlatte ulifanyika siku moja tu baada ya mmoja wa wasaidizi wake, Ernst Lafortune, kufa katika mazingira ya kutatanisha.
Siku kadhaa zilizopita, watumishi wa mahakama wanaochunguza kifo cha Moise, walisema walilazimika kwenda mafichoni baada ya kutishiwa maisha endapo wasingebadilisha baadhi ya majina na maelezo kwenye ripoti zao.
Mkuu wa Chama cha Mahakimu cha Haiti, Jean Wilner Morin, alisema hakushangazwa na uamuzi wa Chanlatte kutokana na kuwepo kwa vitisho kwa mahakimu wanaoteuliwa.
"Nilishasema kuwa hili lingekuwa jambo gumu kwa Jaji Chanlatte: bado ana gari ile ile, hana maafisa wa ziada wanaomlinda," aliliambia shirika la habari la AFP.
"Makundi yenye silaha yapo karibu sana na ilipo Mahakama ya Mwanzo ya Port-au-Prince, kwa hivyo ni vigumu kwa hakimu yeyote kuendelea na kesi hii," aliongeza.
Hakuna ulinzi kwa majaji
Waziri wa Sheria na Usalama wa Umma, Rockefeller Vincent, alisema wizara yake ingelikuwa hatua zote muhimu kuhakikisha usalama wa majaji na mashahidi.
Lakini Wilner Morin alisema kukosekana kwa hakikisho la usalama kilikuwa kikwazo kikubwa kwa kesi hiyo.
"Pale hakimu anapokuwa hapewi nyenzo muhimu za kuishughulikia kesi kama hii, kunaizuwia kesi yenyewe.
Polisi wanasema wamewakamata watu 44 wakiwahusisha na mauaji hayo, wakiwemo maafisa 21 wa polisi wa Haiti, raia 18 wa Colombia wanaoshukiwa kuwa kwenye kikosi cha makamando, na raia wawili wa Kimarekani wenye asili ya Haiti.
Mkuu wa kikosi cha usalama cha Moise ni mmoja wa wanaoshikiliwa akiunganishwa na njama iliyoandaliwa na raia wa Haiti wenye mafungamano na raia wa kigeni.
Polisi imetangaza pia kuwasaka watu wengine kadhaa, akiwemo jaji mmoja wa mahakama ya juu, seneta wa zamani na mfanyabiashara mmoja.
Moise aliuawa wakati washambuliaji walipoingia kwenye nyumba yake tarehe 7 Julai na kumpiga risasi. Mkewe, Martine, alijeruhiwa vibaya lakini alipona.
Alikuwa analiongoza taifa hilo masikini na linalokumbwa na majanga ya mara kwa mara akitumia dikrii, wakati ghasia za makundi yenye silaha zilipozuka na virusi vya corona kuzidi kusambaa.