Jamhuri ya Afrika ya Kati yaomba msaada wa Ufaransa
27 Desemba 2012Mamia ya watu wamekusanyika jana nje ya ubalozi wa Ufaransa wakiwasilisha ombi hilo, ambalo Ufaransa haijajibu haraka lakini imesema wanajeshi zaidi wa kulinda amani wametumwa kuweka ulinzi katika ubalozi huo. Hayo yanajiri wakati Umoja wa Mataifa na Marekani wakiwataka raia wao kuondoka nchini humo.
Ban ameomba usitishwaji mapigano
Ripoti zinasema kwamba muungano wa waasi wa Seleka umeiteka miji kadhaa katika wiki za karibuni wakati waasi hao wakisonga mble kwa kasi kuelekea mji mkuu Bangui. Muungano huo wa Seleka unasema unapambana kutekeleza mpango wa amani ili kusitisha uasi uliofanywa awali au utamwondoa rais aliyeko madarakani Francois Bozize. Umoja wa Mataifa jana Jumatano umewashutumu waasi hao kwa kusonga mbele na kuamuru zaidi ya wafanyakazi wake 200 na familia zao kuondoka nchini humo. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Martin Nesirky ametoa taarifa inayosema Ban amelaani kabisa mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha dhidi ya miji kadhaa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kupangwa na muungano wa waasi SELEKA.
Anasema hali hii inahujumu kwa kiasi kikubwa mikataba ya amani Iliyopatikana, pamoja na juhudi za jamii ya kimataifa kutafuta amani nchini humo. Nesirky pia amethibitisha kuwa familia zote za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wasiokuwa na majukumu makubwa zimehamishwa kutoka nchini humo. Mwakilishi maalum wa Ban, nchini humo Margaret Vogt anaendelea kuzungumza na serikali na viongozi wa waasi kwa lengo la kuhakikisha usitishwaji vita na kuanzisha mazungumzo.
Waasi wanasonga mbele
Hatua zilizopigwa na waasi katika wiki za karibuni ambapo wametwaa miji kadhaa zimeangazia ulegevu uliopo katika nchi hiyo, ambayo ina utajiri wa madini ya uranium na dhahabu na almasi lakini haijakuwa imara tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka wa 1960.
Duru za jeshi zinasema waasi wamesonga hadi mji wa Damara, kilomita 75 kutoka mji mkuu Bangui, kufikia jana mchana, baada ya kuudhibiti mji wa Sibut ambako takribani wanajeshi 150 wa Chad awali walikuwa wamewekwa kujaribu kuwazuia waasi dhidi ya kuingia upande wa kusini.
Nchi kadhaa za Afrika ya Kati zina vikosi vyao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kama sehemu ya ujumbe wa MICOPAX, na Chad iliongeza idadi ya wanajeshi wake mapema mwezi huu. Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema badhii ya wanajeshi wakem 250 walioko nchini humo kama sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa MICOPAX wametumwa kuweka ulinzi katika ubalozi wao na kuwalinda raia wa Ufaransa. Marekani pia imetoa wito wa kufanywa mazungumzo wakati ikiwataka raia wake kuondoka nchini humo hadi pale hali ya usalama itakapoimarishwa. Safari ya ndege ya kila wiki ya kampuni ya Air France kutoka Paris hadi Bangui imelazimika kugeuza mkondo kutokana na hali mjini Bangui. Rais Francois Bozize aliingia madarakani mnamo mwaka wa 2003 baada ya vita vya muda mfupi na kila mara yeye hutegemea uingiliaji wa kigeni kupambana na uasi na ukosefu wa usalama nchini humo unaotokana na migogoro ya nchi jirani.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Hamidou Oummilkheir