1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii ya kimataifa yataka Afghanistan kuendeleza mazungumzo

23 Juni 2021

Mjumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan ameiomba jumuiya ya kimataifa kufanya kila linalowezekana kulishinikiza kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan wanaopambana kurejea kwenye mazungumzo.

https://p.dw.com/p/3vPYJ
Schweiz I UN I Deborah Lyons
Picha: Valentin Flauraud/KEYSTONE/picture alliance

Mjumbe huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Deborah Lyons pia ameonya kwamba kukosekana kwa hatua yoyote kunaweza kusababisha umwagikaji wa damu na mzozo utakaoendelea kwa muda mrefu zaidi. 

Lyons ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba hali ya sasa inamtia wasiwasi mkubwa na kuongeza kuwa masuala muhimu kama ya kisiasa, usalama na mchakato wa mazungumzo ya amani, uchumi, dharura za kiutu a kukabiliana na janga la COVID-19 ni ama yanakuwa na matokeo hasi au hayaendelezwi.

Amesema, kuongezeka kwa machafuko yaliyofanywa na wanamgambo wa Taliban mwaka uliopita na kukwama kwa mazungumzo ya amani yaliyoanza mwezi Septemba huko Qatar lakini pia hatua ya wanamgambo hao kuimarisha kampeni zao za kijeshi, kwa pamoja yamechangia kuongezeka kwa uasi.

Amesema "Zaidi ya wilaya 50 kati ya 370 za Afghanistan zimechukuliwa tangu mwanzoni mwa mwezi Mei. Wilaya nyingi ambazo zimekuwa zichukuliwa ni zile zilizopo karibu na miji mikuu ya majimbo. Hii inamaanisha kwamba Taliban wanajiandaa kujaribu kuchukua miji hiyo mikuu mara baada ya wanajeshi wote wa kigeni kuondoka."

Afghanistan Volksmobilisierung gegen die Taliban
Wanamgambo wa Taliban wanalaumiwa kwa mashambulizi dhidi ya raia na wameanza kujiimarisha zaidi wakati jeshi la kigeni likikaribia kuondoka. Picha: Ministry of Defense

Waziri wa mambo ya kigeni wa Afghanistan Mohammad Haneef Atmar ameliambia baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba watu wa Afghanistan wameshuhudia mashambulizi makali zaidi katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, huku akiwatuhumu wanamgambo wa Taliban kwa kushindwa kuheshimu wajibu wao uliopo kwenye makubaliano ya Februari 2020 na badala yake waliongeza mashambulizi na kuvuruga kabisa ustahimilivu wa taifa hilo na ukanda mzima.

Ameliomba kudi hilo la wanamgambo kuieleza jumuiya ya kimataifa sababu za kuwaua waAfghanistan wenzao na hususan raia, ilhali mwanzoni walidai wanapambana na wanajeshi wa kigeni.

Zikiwa zimesalia wiki kadhaa kwa wanajeshi wote wa Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO kuondoka Afghanistan, Atmar ameisihi jumuiya ya kimataifa kujaribu kuwashawishi Taliban kuheshimu makubaliano hayo na Marekani, yanayokwenda sambamba na maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Marekani kwa upande wake jana Jumanne imetoa mwito wa kumalizwa mapigano nchini Afghanistan huku ikilitupia lawama kundi hilo kwa ongezeko la uasi na umwagikaji mkubwa wa damu, siku tatu kabla ya ziara ya rais Ashraf Ghani nchini Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price amenukuliwa akiziomba pande zinazohasimiana kurudi kwenye mazungumzo yatakayofungua njia ya suluhu la kisiasa kwa ajili ya mustakabali wa taifa hilo.

Siku ya Ijumaa, rais Joe Biden anatarajia kukutana na Ghani na Abdullah Abdullah anayeiwakilisha serikali ya Afghanistan kwenye mazungumzo ya amani na Taliban.

Mashirika: APE/AFPE