Jammeh akubali kuachia madaraka
21 Januari 2017Jammeh alikutana kwa masaa kadhaa na viongozi wa Guinea na Muritania siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Banjul. Hatimaye makubaliano yalifikiwa, ya kwamba atamkabidhi madaraka, Adama Barrow, mgombea aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.
"Nimeamua leo hii nikiwa na fahamu zangu timamu kuachia uongozi wa taifa hili na ninawashukuru Wagambia wote," amesema Yahya Jammeh, katika taarifa iliyorushwa kwenye kituo cha televisheni ya taifa.
Kiongozi huyo amesema uamuzi huo wa kuachia madaraka -- baada ya wiki kadhaa za kugoma kukubali kushindwa kwa kutumia vitisho pamoja na hatua za kisheria -- ulikuwa ni wake peke yake, licha ya kukabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, bado haikuamuliwa ni nchi gani atakayoishi kiongozi huyo baada ya kuachia ngazi ya wadhifa wa urais.
"Uamuzi wangu wa leo haukutokana na sababu nyingine yoyote isipokuwa maslahi yenu wananchi wa Gambia, na na yale ya taifa letu kipenzi," amesema Jammeh katika taarifa yake hiyo huku akiwashukuru raia wa Gambia kwa namna walivyomuunga mkono.
"Katika wakati ambapo tunashuhudia shida na hofu katika maeneo mengine barani Afrika na duniani kote, amani na usalama ni urithi wetu wa pamoja wa Gambia ambao ni lazima kwetu kuulinda na kuutetea," amezidi kueleza Jammeh.
Hatua zake zitakuwa zinafuatiliwa kwa umakini katika masaa na siku zinazofuatia tangazo lake hilo, kutokana na kwamba alishatoa tamko kama hilo la kukubali kushindwa na kumtambua, Adama Barrow, kama mshindi mara tu baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi kutangazwa. Hata hivyo, Jammeh alibadilisha kauli hiyo baadae kwa madai kwamba kulikuwa na hitilafu katika uhesabuji kura.
Awali vikosi vya wanajeshi wa nchi kadhaa za Afrika Magharibi, vilivuka mpaka wa Senegal na kuingia nchini Gambia kwa lengo la kutumia nguvu ili kumuondoa Jammeh madarakani.
Ujumbe wa viongozi wa Afrika Magharibi ikiwa ni pamoja na Rais wa Guinea na Mauritania pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, walimtaka Jammeh kufanya uamuzi wake wa mwisho ifikapo Ijumaa jioni.
Kabla ya hapo, mkuu wa jeshi la ulinzi la Gambia, Ousman Badgi, alisisitiza kwamba hakutakuwepo vita au mapigano ya aina yoyote na kwamba kinachoendelea ni ukosefu wa maelewano ya kisiasa na aliapa kuwa suluhisho pia litakuwa la kisiasa na sio la kijeshi.
Hata hivyo, utata uliojitokeza tokea baada ya Jammeh kukataa kuutambua ushindi wa Barrow, ulisababisha watu wapatao 45,000 kuikimbia nchi, asilimia 75 miongoni mwao wakiwa watoto waliokimbizwa na mama zao au jamaa zao wa kike.
Siku ya Alhamis, Rais Barrow aliapishwa rasmi kuwa rais katika ofisi ya ubalozi wa Gambia nchini Senegal mji mkuu wa Dakar. Barrow alikimbilia nchini humo kwa kuhofia usalama wake.
Gambia ni nchi iliyowahi kutawaliwa na Uingereza, na ni miongoni mwa nchi 20 masikini ulimwenguni, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Ukulima pamoja na utalii ni miongoni mwa vitegemezi vikuu vya uchumi nchini humo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo