Je bunge la Uingereza litaupitisha mpango wa Brexit?
5 Desemba 2018Hayo yakijiri wabunge wa Ungereza jana jioni walipiga kura ya kuwa na maamuzi zaidi iwapo bunge litaukataa mpango huo. Wakati wa kipindi cha maswali kwa waziri mkuu, May alikabiliwa na swali kutoka kwa kiongozi wa chama cha Scotland cha National Party, akitakiwa kueleza kwanini Ireland ya kaskazini itasalia kwenye soko la pamoja la Umoja wa Ulaya na Scotland isiwemo chini ya kile kinachoitwa sera ya uhakikisho.
Hayo yakijiri, wabunge wa Uingereza jana walipiga kura kujipatia maamuzi zaidi, ikitokea kama inavyotarajiwa, mpango wa waziri mkuu Theresa May utakataliwa na Baraza la chini la bunge la Uingereza. Wakati wa mjadala juu ya mpango wa Brexit Jumanne jioni, wabunge kadhaa kutoka chama chake cha Conservative, waliwasilisha muswada wa marekebisho yanayotafuta ushawishi wa nini kitatokea endapo mpango huo utakataliwa bungeni wiki ijayo.
Marekebisho hayo yaliyoungwa mkono na mwanasheria mkuu wa zamani Dominic Grieve miongoni mwa wengine lakini yakapingwa na serikali, yalipitishwa kwenye Baraza la chini la Bunge kwa kura 321 dhidi ya 299. Kama mpango wa Brexit utakataliwa, serikali italazimika kurudi kwenye Baraza hilo ndani ya siku 21 kutoa kauli ya nini kitafuatia.
"Ninahitimisha kwa kuzieleza pande zote za mjadala, kwa kila mwanachama katika kila chama . Ninasema kwamba mpango huo unastahili kuungwa mkono, kwa ajili ya watu wetu wote na Uingereza nzima, muungano mmoja wa mataifa manne sasa na katika siku za usoni, na huu ni mjadala kuhusu mustakabali wa baadae, sio juu ya kama tungeweza kuchukua mwelekeo tofauti katika siku za nyuma lakini ni njia gani tunapaswa kuchukua kutoka hapa," alisema May.
Waziri wa zamani Oliver Letwin aliyeunga mkono marekebisho ya Grieve, alisema kipaumbele kilikuwa ni kuzuia uwezekano wa madhara ya Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya kuwa na makubaliano. Wabunge kimsingi wamegawanyika juu ya uwezekano wa kuwa na aina tofauti za Brexit na wote kutoka chama cha Conservatives na Labour wamejizatiti kuondoka Umoja wa Ulaya. Hata hivyo kila kitu kinaweza kubadilika kama mkataba wa May utakataliwa. Na ikiwa utashindwa, May bado anakabiliwa na kibarua cha kuondolewa madarakani kutoka pande zote.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga