Je, India itamrudisha Sheikh Hasina Bangladesh?
25 Oktoba 2024Baada ya ghasia kali nchini Bangladesh kulazimisha Hasina kuondoka ofisini na kukimbilia India, mahakama hiyo ilitoa hati ya kumkamata, ikidai kuwa anahusika na vifo vya mamia ya wanafunzi na waandamanaji. Mahakama imeamuru Hasina na wenzake 45 kufikishwa mahakamani kufikia Novemba 18 kwa tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya malalamiko 60 yamewasilishwa dhidi ya Hasina na viongozi wengine wa chama chake cha Awami League, wakituhumiwa kwa mauaji na utekaji nyara wa watu.
Bangladesh ina mpango wa kuanzisha mkataba wa usafirishaji wa wahalifu
Hasina alikimbilia India kwa helikopta ya kijeshi tarehe 5 Agosti wakati wa ghasia zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000. Serikali ya mpito ya Dhaka ilifuta hati yake ya kidiplomasia baada ya kukimbia kwake. Hata hivyo, maafisa wa India wanaendelea kumpa hifadhi Hasina chini ya ulinzi mkali katika nyumba salama nje ya New Delhi, ambapo hata binti yake, Saima Wazed, hajafanikiwa kumwona.
India haijaonyesha dalili za kumrudisha Hasina Bangladesh. Huko Dhaka, mshauri wa kisheria wa serikali ya mpito, Asif Nazrul, alisema kuwa Bangladesh itapinga vikali kama India itakataa kumrudisha Hasina, kwani wanadai India ina wajibu chini ya mkataba wa usafirishaji wa wahalifu uliofikiwa mwaka 2013. Hata hivyo, mkataba huo unaruhusu India kukataa usafirishaji ikiwa kosa ni la kisiasa.
India inaendeleza mkakati wa kidiplomasia
Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India wamekuwa wakiepuka maswali kuhusu usafirishaji wa Hasina, wakielezea kuwa alienda India kwa sababu za usalama. Serikali ya India inajaribu kuweka mizani kati ya kujenga uhusiano mzuri na utawala mpya wa mpito huko Dhaka na kuhifadhi uhusiano mzuri ambao Hasina alikuwa ameujenga na India akiwa madarakani.
Wakili wa Mahakama Kuu ya India, Karan Thukral, alisema kuwa uamuzi wa India juu ya Hasina unahitaji kuzingatia majukumu ya kisheria, haki za binadamu, na mikakati ya kidiplomasia.
Hasina anaweza kupinga ombi la usafirishaji huo mahakamani, huku wachambuzi wakibainisha kuwa mchakato huo unaweza kuchukua muda, hasa kutokana na vipengele vya kisiasa vilivyopo kwenye mkataba wa usafirishaji.
Je, Bangladesh inaweza kuitenga India?
Bangladesh ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa India katika Asia Kusini, na biashara kati ya nchi hizo mbili inakadiriwa kuwa $15.9 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022-23. Baada ya mabadiliko ya uongozi huko Dhaka, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameahidi kuendeleza miradi ya maendeleo nchini Bangladesh.
Hata hivyo, kiongozi wa mpito wa Bangladesh, Muhammad Yunus, anakabiliwa na changamoto ya kusaka haki kwa wahanga huku akihifadhi uhusiano wa kiuchumi na kisiasa na India wakati akiandaa uchaguzi mpya unaotarajiwa mwaka ujao.