1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeneza la Malkia Elizabeth laanza safari ya mwisho Scotland

11 Septemba 2022

Safari ya mwisho ya muda wa saa sita ya Jeneza la malkia Elizabeth wa pili imeanza kutoka kwenye makaazi yake ya Scotland

https://p.dw.com/p/4Ggr2
Überführung von Queen Elizabeth II
Picha: Hannah McKay/REUTERS

Safari ya mwisho ya muda wa  saa sita ya Jeneza la malkia Elizabeth wa pili imeanza  kutoka kwenye makaazi yake ya Scotland kuelekea mji mkuu Edinburgh leo Jumapili huku  umati wa watu ukiwa umejipanga  kando kando ya barabara kutoa heshima za mwisho kwa malkia huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 96.

Beerdigung von Queen Elizabeth II
Picha: Hannah McKay/REUTERS

Mchakato huo ni sehemu ya kwanza ya msururu wa matukio ya kuomboleza msiba huo utakaokamilishwa kwa maziko ya kiongozi huyo mnamo tarehe 19 mwezi huu wa Septemba.Jeneza lililobeba maiti ya Malkia limefunikwa bendera maalum ya kifalme ya Scotland na kupambwa juu kwa shada la maua. Gari maalum lililobeba maiti yake liliondoka kwenye kasri la Balmoral na kuelekea mji mkuu wa Scotland saa chache zilizopita.

Kifo cha malkia Elizabeth wa pili kimewaliza watu wengi,kusababisha majonzi na kushuhudiwa salamu za rambi rambi za huzuni zikitolewa na watu mbali mbali sio tu na familia ya malkia huyo bali na hata waingereza wengi kwa ujumla wao na duniani.Malkia huyo wa Uingereza ameongoza taasisi hiyo ya kifalme katika jukwa la dunia kwa miongo saba.Malkia Elizabeth aliitangazwa malkia baada ya kifo cha baba yake mfalme Goerge wa sita mnamo Februari 6 mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 25.Sherehe ya kumtawaza rasmi ilifanyika mwaka uliofuatia.

Überführung von Queen Elizabeth II
Picha: Hannah McKay/REUTERS

Elizabeth Alexander,mwenye umri wa miaka 69 ni mwanamama aliyezaliwa siku ambayo Malkia Elizabeth alipotawazwa mwaka 1953 hivi sasa ana umri wa miaka 69 ni miongoni mwa waingereza waliojitokeza katika kijiji cha Ballater kilichoko karibu na makaazi ya Balmoral,kusubiri jeneza la malkia hiyo likipita.Amesema ni jambo la huzuni kwa mtu yoyote kusema kwaheri na anajihisi kama anamuaga kwa mara ya mwisho mtu wa familia,ni jambo linalompa huzuni kutambua malkia hatokuwa nao tena.

Binti wa malkia Elizabeth wa pili,mwanamfalme Anne anaandamana na jeneza hilo ambalo litatembezwa kwa mwendo wa taratibu kutoka kasri lake la Balmoral na kupitia miji midogo midogo na vijiji kadhaa hadi katika mji mkuu wa Scotland,Edinburgh ambako jeneza hilo litawekwa katika eneo maalum kwenye kasri la Holyroodhouse. Safari hiyo ya jeneza la malkia huko Scotland ni moja ya msururu wa matukio ya kuelekea maziko ya malkia huyo mjini London tarehe 19 Septemba itakayotangazwa siku ya mapumziko nchini Uingereza.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW