1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jerusalem. Annan ataka azimio la umoja wa mataifa litekelezwe.

30 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDGi

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan amesema kuwa amani ya kudumu baina ya Israel na Hizbollah inawezekana iwapo azimio la umoja wa mataifa juu ya Lebanon litatekelezwa kikamilifu.

Matamshi yake yamekuja katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Jerusalem na waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Tzipi Livni.

Annan alikutana hapo kabla na waziri mkuu Ehud Olmert ambae pia alieleza matumaini yake kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na umoja wa mataifa yanaweza kulifikisha eneo hilo katika enzi mpya za mahusiano na Lebanon, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya nchi hiyo.

Annan amesema kuwa anamatumaini ya kuongeza idadi ya wanajeshi wa umoja wa mataifa nchini Lebanon hadi kufikia 5,000 katika muda wa siku ama wiki kadha.

Hii amesema itasaidia Israel kuondoa hali ya kuizingira Lebanon.

Bwana Annan na Olmert pia wametoa wito wa kuachiliwa kwa wanajeshi wawili wa Israel ambao wanashikiliwa nchini Lebanon. Kukamatwa kwa watu hao Julai 12 kulizusha mapigano ya mwezi mzima baina ya Israel na Hezbollah.

Wakati huo huo rais wa Palestina Mahmoud Abbas amemwambia katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan leo kuwa hakutakuwa na amani ya kudumu katika mashariki ya kati hadi pale Israel itakapositisha ukaliaji kwa mabavu maeneo ya Wapalestina na kuundwa kwa taifa hilo. Ameongeza kuwa kuendelea kukalia ardhi ya Waarabu na ya wapalestina hakutaleta amani.

Usalama na uiamara vinaweza kupatikana pale tu kutakapokuwa na uhakika wa kurejeshwa kwa haki za kisheria kwa Wapalestina, utekelezaji wa maazimio ya sheria za kimataifa, uundwaji wa taifa huru la palestina na Jerusalem ya mashariki ikiwa ndio mji mkuu na kutatua masuala ya wakimbizi wa Kipalestina.