JERUSALEM. Palestina yasema mkutano na Israel haukuafikia malengo waliyotarajia
22 Juni 2005Utawala wa Palestina umetoa masikitiko yake kufuatia mkutano wa rais Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon mjini Jerusalem.
Waziri mkuu wa Palestina Ahmed Qurie akisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa mkutano baina ya viongozi hao ulikuwa mgumu na haukuonyesha dalili za mafanikio waliyo yatarajia.
Kwa upande wake waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon amesema kuwa yeye na rais Mahmoud Abbas wamekubaliana kudumisha ushirikiano katika mpango wa Israel wa kuihama Gaza, lakini akakasisitiza kuwa hakuna la muafaka litakalo zingatiwa juu ya maswala ya amani mpaka utawala wa Palestina utakapo wajibika kikamilifu katika hatua ya kumaliza mashambulizi ya vikundi vya wanamgambo wa kipalestina wenye msimamo mkali.
Kabla ya mkutano huo kuanza hapo jana walinda usalama wa Israel waliwakamata takriban wanachama 50 wa kundi la Islamic Jihad katika ukingo wa magharibi kufuatia mashambulizi ya mfululizo ambayo inaaminika yalifanywa na kundi hilo.
Wakati huo huo takriban watu saba wameuwawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ajali ya gari moshi lililokuwa likisafiri kutoka mji wa Tel Aviv kuelekea kusini mwa Israel kugonga lori katika mji wa Kiryat Gat. Polisi wamesema watu wengine bado wamekwama ndani ya vifusi vya mabehewa yalioanguka.