JERUSALEM : Viongozi wa Israel na Palestina kukutana
3 Oktoba 2005Waziri Mkuu wa Israel Ariel Sharon na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina wamekubaliana kuwa na mkutano wa viongozi hivi karibuni wakati wakibadilishana salamu za kuadhimisha mwaka mpya wa Kiyahudi na mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa Waislamu.
Sharon na Abbas ilikuwa wamepanga kukutana hapo jana Jumapili lakini mkutano huo ulifutwa wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina wiki iliopita. Ofisi ya Sharon imeripoti kwamba viongozi hao wawili wamekubali kuimarisha ushirikiano pamoja na kuchukuwa hatua za kuuendeleza mchakato wa amani.
Israel ilikuwa imesitisha mashambulizi yake ya kijeshi ya wiki moja katika Ukanda wa Gaza baada ya makundi ya wanamgambo ya Hamas na Islamik Jihad kutangaza kukomesha kwa mashambulizi ya roketi nchini Israel.