JERUSALEM:Viongozi wa Israel na Palestina wakutana
15 Aprili 2007Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas wanafanya mazungumzo hii leo ili kujaribu kumaliza tofauti zao na kuweza kupata suluhu .Viongozi hao hawaonekani kufikia mwafaka wowote ili kufikia makubaliano ya kutafuta amani ya eneo la Mashariki ya Kati.
Mazungumzo hayo yatakayofanyika katika makazi ya Bwana Olmert mjini Jerusalem ni ya kwanza tangu viongozi hao kukubaliana kukutana kila baada ya majuma mawili baada ya mkutano na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Bi Condoleeza Rice.
Kulingana na washauri wa Bwana Olmert mkutano huo unajadilia masuala ya kiuchumi,kisheria na mpango mzima wa serikali ya taifa la Palestina litakaloundwa.Serikali ya kitaifa ya Palestina iliundwa mwezi jana na kushirikisha vyama vya Hamas na Fatah.
Hata hivyo kwa upande mwingine,masuala muhimu yanayohusu mipaka ya taifa la Palestina,hatma ya Jerusalem vilevile mustakabal wa wakimbizi wa Palestina hayatazungumziwa katika kikao hicho.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwa upande wake anatilia mkazo kufanyika kwa majadiliano yatakayowezesha Israel kuerejesha ardhi ya mataifa ya Kiarabu inayokalia kama ilivyopendekezwa na mataifa ya Kiarabu.