1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Jeshi la Israel laashiria kushambulia Kusini mwa Gaza

17 Novemba 2023

Jeshi la Israel limeaashiria kuwa litaelekeza mashambulizi yake eneo la kusini ambako iliamuru wakaazi wa Gaza kuhamia kutafuta hifadhi kutoka maeneo ya kaskazini

https://p.dw.com/p/4Yyad
Majengo yalioporomoka kutokana na mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023
Majengo yalioporomoka kutokana na mashambulizi ya Israel katika ukanda wa GazaPicha: Bashar Taleb/APA/ZUMa/picture alliance

Jeshi hilo limeaashiria litaelekeza mashambulizi yake eneo la kusini ambako iliamuru wakaazi wa Gaza kuhamia kutafuta hifadhi kutoka maeneo ya kaskazini. Limesema baada ya operesheni kubwa kwenye hospitali ya Al-Shifa na mapambano ya wiki tano kaskazini mwa Gaza, sasa limechukua udhibiti kwa sehemu kubwa wa eneo hilo. Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amearifu kuwa sasa malengo ya jeshi la nchi hiyo ni pamoja na maeneo ya kusini akisema "watawasambaratisha wapiganaji wa Hamas popote walipo."

Soma pia:Palestina yahofia maisha ya walionasa hospitali ya Al-Shifa

Vikosi vya nchi hiyo vimesambaza vipeperushi kutokea angani vikiwataka Wapalestina wanaoishi kwenye mji wa kusini wa Khan Younis kuondoka. Vipeperushi sawa na hivyo vilitolewa hapo kabla kaskazini mwa Gaza wiki kadhaa kabla ya kutumwa vikosi vya ardhi vya Israel. Sambamba na hayo mashambulizi ya Israel bado yameendelea siku nzima jana alhamisi.

Kwenye mji wa Deir al-Balah kulifanyika mazishi ya watu 28 waliouwawa kwenye hujuma za ndege za Israel usiku wa kuamkia jana. Majengo na miundombinu mingine imeharibiwa vibaya.

Mazungumzo ya kusitisha vita katika ukanda wa Gaza yanaendelea

Wakati hayo yakijiri imearifiwa kuwa mazungumzo ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa wanawake na watoto wanaoshikiliwa mateka na kundi la Hamas yanaendelea. Hayo ni kulingana duru za habari zinazofuatilia kwa karibu suala hilo.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tel Aviv mnamo Oktoba 30. 2023
Waziri mkuu wa Israel - Benjamin NetanyahuPicha: imago images/Xinhua

Taarifa hizo zimeripotiwa pia na shirika la habari la DPA. Makubaliano hayo ya kuwaachilia baadhi ya mateka yanatarajiwa kufanikisha kusimamishwa kwa mapigano kwa siku 3 hadi tano, kuongezwa kwa misaada ya kiutu pamoja na kuachiliwa kwa wanawake na watoto wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel.

Soma pia:Baraza la usalama la UN latoa wito wa kurefushwa kwa usitishaji mapigano katika ukanda wa Gaza

Kwa mujibu wa vyanzo vyenye ufahamu na mazungumzo hayo, kundi la Hamas limekubaliana na masuala yaliyoainishwa likiwemo la kuwaachia wanawake 50 wanaoshikiliwa mateka na watoto. Kwa kufanya hivyo, Israel itawaachilia wanawake na watoto  75 wa Kipalestina. Lakini bado hakuna taarifa za uhakika juu ya ni lini hasa makubaliano yatatekelezwa.

Waandamanaji nchini Marekani wato wito wa kusitishwa kwa vita Gaza

Huko nchini Marekani mamia ya waandamanaji wanaotaka mapigano yasitishwe kwenye Ukanda wa Gaza waliziba madaraja muhimu ya ikiwemo kwenye njia kuu ya kuingia mji wa San Francisco kunakoendelea mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Asia na Pasifiki, APEC. Viongozi kadhaa ikiwemo rais Joe Biden wa Marekani wanahudhuria mkutano huo.

Zaidi ya waandamanaji 50 wamekamatwa na magari 15 yalitiwa nyonyoro na kuondolewa barabarani yakihusishwa na kuzuia barabara.

Inakadiriwa idadi ya waandamanaji walifikia 200 na walishika mabango yenye ujumbe wa "sitisha mapigano sasa" wakimtaka rais Biden na viongozi wa APEC watoe tamko la kusitisha vita Ukanda wa Gaza.