1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel laondoa vizuizi karibu na Gaza

6 Mei 2019

Jeshi la Israel limeondoa vizuizi karibu na eneo la Gaza kusini mwa Israel, huku Hamas ikiripoti kuwa mpango wa kusitisha mapigano umefikiwa ili kumaliza mapigano kati ya pande hizo mbili tangu vita vya mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/3I1IT
Gaza-City Zerstörungen nach Luftangriffen aus Israel
Picha: Reuters/S. Salem

Mapigano hayo ya siku mbili yamewaua watu 23 kwa upande wa Gaza, wakiwemo wapiganaji na raia, huku kwa upande wa Israel raia wawili wameuawa.

Kundi la jihadi la Hamas linaloitawala Gaza na ambalo Israel inalishutumu kwa kuchochea ghasia za sasa, limethibitisha kwamba makubaliano yamefikiwa chini ya usimamizi wa Misri. Miongoni mwa watu 23 waliouawa ni pamoja na wapiganaji tisa, wanawake wawili wajawazito pamoja na watoto wawili.

Utulivu warejea

Wizara ya usafiri ya Israel imetangaza kuwa usafiri wote wa umma katika eneo la kusini mwa nchi hiyo utarejea na shughuli zitaendelea kama kawaida. Njia ya reli kati ya miji ya Ashkelon na Beersheba ilitarajiwa kuanza kutumika tena kesho asubuhi. Aidha, mabenki kwenye eneo hilo tayari yamefunguliwa baada ya kufungwa kwa siku tatu, ingawa shule zitafunguliwa kesho asubuhi.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amesema wapatanishi wa Misri, wakisaidiana na wajumbe kutoka Qatar na Umoja wa Mataifa wameyafanikisha makubaliano hayo ili kuituliza hali ya mambo.

''Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza baada ya wapatanishi kuingilia kati na tunaliangalia hili suala la kuyakalia maeneo jinsi linavyoendelea na tuko tayari kujibu mashambulizi iwapo utafanyika uchokozi wa aina yoyote ile. Suala la ukaliaji lazima liendane na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na pande zinazohasimiana,'' alisema Qassem.

Mashambulizi yalianza mwishoni mwa wiki

Qassem amesema mashambulizi yalianza Jumamosi kutoka Gaza, na Israel ikarusha makombora ya kujibu na mashambulizi hayo yakaendelea hadi jana Jumapili.

Israel Gaza l Auto wurde von einer Rakete in der Nähe von Yad Mordechai im Süden Israels getroffen
Wanajeshi wa Israel wakiweka doria kusini mwa IsraelPicha: Getty Images/AFP/J. Guez

Wapiganaji wa Kipalestina walifyatua mamia ya roketi kuelekea Israel, huku jeshi la Israel likijibu mashambulizi katika maeneo yapatayo 350 ya wapiganaji ndani ya Gaza. Maeneo yaliyolengwa na Israel ni pamoja na maghala ya kuhifadhia silaha, mahandaki pamoja na maeneo ya kutengeneza maroketi.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema wazi kuwa operesheni bado haijamalizika na inahitaji uvumilivu zaidi. Israel na Hamas wamekuwa maadui wakubwa na wamepigana vita vya miaka mitatu na mashambulizi mengine madogo madogo tangu kundi hilo la jihadi lilipoidhibiti Gaza mwaka 2017.