Jeshi la Israeli lashambulia washukiwa wa wanamgambo, Syria
3 Agosti 2020Msemaji wa jeshi la Israeli, Luteni kanali Jonathan Conricus, amesema kuwa mapema wanajeshi wa nchi hiyo walikuwa wamevamiwa kufuatia shughuli zisizokuwa za kawaida katika eneo la milima la Golan. Conricus amesema wanajeshi hao waliwafyatulia risasi washukiwa wa wanamgambo baadhi yao wakiwa wamejihami baada ya kuwafuatilia wakitega vilipuzi ardhini.
Jeshi hilo lilitoa video iliyowaonesha washukiwa wanne wakikimbia kabla ya kupotea katika mlipuko uliosababishwa na shambulizi hilo.Jeshi hilo la Israeli bado halijabainisha iwapo washukiwa hao wanne wana ushirikiano na Iran ama kundi la wanamgambo la Hezbollah ambao ni washirika wakuu wa Syria.
Hata hivyo Conricus amesema kuwa serikali ya Israeli inailaumu serikali ya Syria kwa shambulizi hilo.Shirika la habari la serikali ya Syria SANA halikuthibitisha mara moja kuhusu shambulizi hilo la Israeli.Israeli iliteka eneo hilo la milima la Golan mnamo mwaka 1967 na baadaye kulikalia kwa kutumia nguvu. Marekani ndilo taifa la pekee linalotambua mamlaka ya Israel katika eneo hilo.Tukio hilo linajiri huku hofu ikiongezeka katika eneo la Kaskazini la Israeli kufuatia shambulizi la angani lililosababisha kifo cha mpiganaji mmoja wa kundi la wanamgambo la Hezbollah nchini Syria.Kufuatia shambulizi hilo, eneo la milima la Golan lilishambuliwa na vilipuzi kutoka Syria na Israel ikajibu kwa kushambulia maeneo ya kijeshi ya Syria na kuimarisha vikosi vyake katika eneo hilo.
Wapiganaji 12 wa serikali ya Syria wauawa
Wakati huo huo, Shirika la linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema kuwa makundi ya itikadi kali na washirika wake katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Syria, leo yamewauwa wapiganaji 12 wa serikali ya nchi hiyo na kutibua operesheni yao.
Shirika hilo limeendelea kusema kuwa wapiganaji wengine 17 walijeruhiwa huku wapiganaji sita wa makundi hayo ya itikadi kali wakiuawa. Vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad wa Syria vilifanya mashambulizi kwa kutumia mizinga mikubwa katika ngome kuu ya mwisho ya upinzani. Lakini muungano wa makundi ya itikadi kali wa Hayat Tahrir-al-Sham HTS unoongozwa na waliokuwa viongozi wa kundi lililokuwa na mafungamano na al-Qaeda la Syria na washirika wake unaripotiwa kutibua mashambulizi hayo.
Muungano huo wa HTS pia unadhibiti maeneo makubwa ya mkoa wa Idlib na maeneo mengine madogo katika mikoa jirani ya Allepo na Hama. Vita nchini Syria ambavyo vimedumu kwa muda wa miaka tisa sasa, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 380,000 na kusababisha takriban nusu ya idadi ya watu nchini humo kupoteza makazi yao.