Jeshi la Kongo lazuia jaribio la mapinduzi
19 Mei 2024Msemaji wa jeshi hilo Sylvain Ekenge ameyasema hayo katika hotuba yake kupitia televisheni ya taifa.
"Jaribio la kuipindua serikali limezuiwa na vikosi vya ulinzi. Jaribio hilo limehusisha Wakongomani na wageni. Watu hao, akiwemo kiongozi wao, hawakupata nafasi ya kusababisha madhara," ameeleza Sylvain Ekenge.
Msemaji huyo wa jeshi hata hivyo hakuweka wazi iwapo watu hao wenye silaha waliuawa au walikamatwa.
Soma pia: Watu saba wauawa katika shambulizi mashariki ya Kongo
Mapema leo, watu watatu wakiwemo walinzi wawili na mshambuliaji mmoja waliuawa katika shambulio kwenye maakazi ya mwanasiasa Vital Kamerhe, mbunge anayewania kiti cha spika wa bunge la taifa.
Mapigano yaliripotiwa kati ya watu wenye silaha waliovalia sare za jeshi na walinzi wa mwanasiasa huyo kwenye makaazi yake yaliyoko eneo la Tshatshi Boulevard, takriban kilomita mbili karibu na Ikulu ya nchi hiyo na baadhi ya ofisi ya balozi za kigeni.
Msemaji wa Vital Kamerhe, Michel Moto Muhim, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, mwanasiasa huyo na familia yake wako salama na kwamba ulinzi wao hivi sasa umeimarishwa.
Mivutano ndani ya chama tawala juu ya nafasi ya uspika
Jaribio hilo la mapinduzi linatokea katikati ya mivutano ndani ya chama tawala cha Rais Felix Tshisekedi juu ya nafasi ya kiti cha spika wa bunge la taifa katika uchaguzi uliopangwa kufanyika jana Jumamosi na ambao umeahirishwa.
Vyombo vya habari vya ndani vimesema waliohusika na shambulio hilo ni wanajeshi wa Kongo. Hata hivyo, haikuwa wazi iwapo watu hao waliovalia sare za jeshi walikuwa wakijaribu kumkamata Vital Kamerhe.
Picha za video, zilizoonekana kutoka eneo la tukio, zimeonyesha malori ya kijeshi na watu wenye silaha wakipita karibu na makaazi ya mwanasiasa huyo.
Soma pia: Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo
Mnamo siku ya Ijumaa, Rais Felix Tshisekedi alikutana na wabunge na viongozi wa chama tawala katika jaribio la kuutatua mzozo ndani ya chama hicho.
Tshisekedi alikwenda mbali zaidi na kutishia kulivunja bunge na kumrudisha kila mtu nyumbani kwenye uchaguzi mpya iwapo kile alichokiita "mazoea mabaya” yataendelea.
Kiongozi huyo alichaguliwa tena kuwa rais mnamo mwezi Disemba katika uchaguzi uliogubikwa na madai ya wizi wa kura.
Ubalozi wa Marekani nchini Kongo ulitoa tahadhari ya usalama na kuwahimiza watu kuwa macho kufuatia ripoti za kutokea makabiliano ya risasi.