1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Mali latuhumiwa kuwauwa raia

Saleh Mwanamilongo
20 Aprili 2021

Shirika la Human Rights Watch limewataka viongozi wa Mali kuchunguza tuhuma za mauwaji na unyanyasaji uliofanywa na jeshi lake katikata mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3sI4M
Mali I  Demonstration gegen Regionalblock ECOWAS in Bamako
Picha: Reuters/M. Kalapo

Shirika la Human Rights watch linasema wanajeshi wa Mali waliwauwa watu wasiopunguwa 34, kulazimika kutoweka kwa watu wasiopunguwa 16 na kuwatesa wafungwa kadhaa wakati wa operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi kwenye jimbo la Mopti, katikati mwa nchi.

 Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeitaka serikali ya mpito nchini humo kuendesha uchunguzi wa kina kufuatia tuhuma hizo. Visa hivyo vilitokea tangu kutokea kwa mapindizu ya kijeshi ya Agosti 18, mwaka 2020.

Uhalifu unapunguza imani ya raia

Kanali Assimi Goita,naibu rais wa Mali na kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 2020
Kanali Assimi Goita,naibu rais wa Mali na kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 2020Picha: Reuters/M. Rosier

Corinne Dufka, mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights watch kwenye ukanda wa Sahel amesema vikosi  vya usalama vya Mali havikuheshimu haki za maisha kwa raia wa Mopti wakati wa operesheni zake za kijeshi dhidi ya ugaidi.

''Kufanya uhalifu kwa madhumuni ya kuhakikisha usalama kunachochea vijana kujiunga na makundi ya wapiganaji ambayo pia yanafanya uhalifu. na kunapunguza imani ya raia wa maeneo hayo,'' alisema Dufka.

Serikali ilitangaza kuanzisha uchunguzi wa visa hivyo kwenye miji ya Libé a Kobou, lakini famili za wahanga zililiambia shirika la Human Rights Watch kuwa viongozi hawakuwasiliana nao.

Human rights watch imewataka waendesha mashitaka wa kijeshi nchini Mali kuendesha uchunguzi huru kufuatia tuhuma hizo na kuwaachisha kazi maafisa waliohusika na visa vya uhalifu.

Visa vya mauaji ya jeshi dhidi ya raia

Wanajeshi wa mali wametuhumiwa kuhusika na visa vya uhalifu dhidi ya raia
Wanajeshi wa mali wametuhumiwa kuhusika na visa vya uhalifu dhidi ya raiaPicha: picture-alliance/AA/H. Kouyate

Kuanzia Novemba hadi April mwaka huu, Shirika la Human Rights watch liliwahoji watu 43 wengine kwa njia ya simu kuhusu visa saba tofauti ambavyo wanajeshi walihusika na uhalifu.

Miongoni mwao ni mashahidi, viongozi wa jamii, wawakilishi wa serikali na wanadiplomasia wa kigeni. Visa hivyo vya uhalifu viliripotiwa kwenye vijiji vya Boni, Feto Hore Niwa, Kobou, Libé, Solla, Sokoura na kwenye  vitongoji vyake.

Mashahidi wameliliambia shirika la Human Rights watch kuwa Machi 23, kwenye mji wa Boni, wanajeshi waliwashikilia watu kadhaa waliokuwa wakisafiri kwa basi, baada ya kukuta vifaa vya kijeshi kwenye basi lao.

Baadae wanajeshi hao waliwafunga macho kwa vitambaa na kisha kuwauwa kwa risasi. Na wasafiri wengine wasiopunguwa 13 walitoweka.

Chanzo: HRW